Home BUSINESS WAHITIMU CHUO CHA BoT WAASWA KUWA WAADILIFU NA WAZALENDO

WAHITIMU CHUO CHA BoT WAASWA KUWA WAADILIFU NA WAZALENDO

Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, akielezea jambo katika shehere za mahafali ya pili ya Chuo cha BoT yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo jijini Mwanza.

Wahitimu pamoja na wageni waalikwa wakiwa katika shehere za mahafali ya pili ya Chuo cha BoT yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Utawala na Udhibiti wa Ndani), Bw. Julian Banzi Raphael, akizingumza katika shehere za mahafali ya pili ya Chuo cha BoT yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo jijini Mwanza.

Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Nicas Yabu, akizingumza katika shehere za mahafali ya pili ya Chuo cha BoT yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo jijini Mwanza.

Wahitimu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) waliotunukiwa Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki na Stashahada ya Uzamili katika Uongozi wa Benki wameaswa kulitumikia taifa kwa uadilifu na uzalendo mkubwa.

Rai hiyo imetolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, ambaye alikua mgeni rasmi katika sherehe za mahafali ya pili ya Chuo cha BoT yaliyofanyika Novemba 17, 2023 jijini Mwanza.

Gavana Tutuba alisema kuwa kwa sasa kuna tatizo la uadilifu na kukosa uzalendo kuliko tatizo la kukosa elimu.

“Wapo baadhi ya watu katika sekta ya fedha ambao wamekuwa wakifanya vitendo visivyo na weledi wala uadilifu na kusababisha hasara na kupungua kwa ufanisi wa sekta ya fedha, ikiwemo uwepo wa mikopo chechefu.

Nawasihi sana msiwe miongoni mwa hao na badala yake muwe mfano wa kuigwa,” alisema. Gavana Tutuba alisisitiza kuwa Benki Kuu inaendelea kuwafuatilia kwa karibu wafanyakazi wote wa sekta ya fedha na haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo visivyokubalika.

Aidha, alisema wahitimu hao wanajukumu la kuwa wabunifu, wachapakazi na kutumia ipasavyo ujuzi na elimu waliyoipata ili kuleta maendeleo kwao binafsi, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla.

“Dunia ya sasa ni ya ushindani na inahitaji watu wenye ubunifu. Msipobuni namna za kutatua changamoto za watu wetu kwenye sekta ya fedha na kwingineko, elimu yenu inaweza isiwasaidie sana,”alisema. Pia, aliwakumbusha wahitimu kuwa suala la kujiendeleza kitaaluma na kitaalam ni muhimu sana katika dunia ya sasa, kwani teknolojia na maarifa vinabadilika kila kukicha.

Hii husababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi, kisayansi, ongezeko la watu na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Nawahimiza kuwa kuhitimu kwenu siku ya leo kuwe ni chachu na mwanzo wa safari mpya ya kujifunza na kupata maarifa mapya katika maeneo na viwango mbalimbali,” alisema Gavana Tutuba.

Gavana Tutuba amekitaka Chuo hicho kutoa mafunzo na kufanya kazi zake katika viwango vya kimataifa ili kukifanya kuwa moja ya vyuo mahiri duniani na programu zake ziendane na mahitaji na mazingira ya sasa ya kimkakati katika Sekta ya Fedha kwa kujumuisha matumizi ya teknolojia.

“Pamoja na wigo mpana uliopo, naendelea kusisitiza kuwa Chuo kiendelee kutoa mafunzo katika nyanja za Sekta ya Fedha tu, Benki Kuu ya Tanzania ipo tayari kuwaunga mkono kujitanua kwa kutoa mafunzo katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na uboreshaji wa Sekta ya Fedha,” alisisitiza.

Gavana Tutuba ameiagiza Bodi ya Chuo kuangalia namna ya kutoa vyeti vya umahiri wa kiithibati katika maeneo mengine kama vile Maduka ya Ubadilishaji wa Fedha (Bureau de Change) na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), ili kuwajengea uwezo wafanyakazi wa maeneo hayo

Awali, Mkuu wa Chuo cha BoT, Dkt. Nicas Yabu, alisema kuwa takwimu za wanafunzi waliohitimu Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki mwaka jana 2022 zinaonesha kuwa kati ya wahitimu 36, wahitimu 21 (asilimia 58.3) wanaendelea na masomo ya vyuo vikuu, wahitimu 14 (asilimia 38.0) wameajiriwa na kujiajiri, na mhitimu mmoja (asilimia 2.7) anaendelea kutafuta kazi.

“Takwimu hizi kwetu ni mafanikio makubwa, tena ya kujivunia. Kwani, hata asilimia kubwa ya walioendelea na masomo ya elimu ya juu imetokana na kunolewa na kuandaliwa vizuri na Chuo chetu,” alisema Dkt. Yabu.

Katika mahafali hayo, wahitimu ishirini na sita (26) wametunukiwa Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki (Ordinary Diploma in Banking Practice and Supervision) ambao kati yao, wanaume ni kumi na mbili (12) na wanawake ni kumi na nne (14).

Vilevile, Wahitimu thelathini na tano (35) wametunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Uongozi wa Benki (Postgraduate Diploma in Banking Management) ambao kati yao, wanaume ni kumi na tatu (13) na wanawake ni ishirini na mbili(22).

Previous articleHABARI KUBWA MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 18-2023
Next articlePROGRAMU YA MAZOEZI KWA WATUMISHI WA WIZARA YAANZA KWA KISHINDO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here