Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini, Faraja Ng’ingo alisema kuwa benki hiyo imekuja na kampeni hiyo ili kuendelea kuhamasisha matumizi ya huduma za benki kwa wakulima na vyama vya msingi.
Alisema NMB inatambua na kuuthamini mchango mkubwa wa biashara ya kilimo kwa kanda ya kusini hususani kilimo cha korosho katika ustawi wa benki hiyo na kanda ya kusini hususan mikoa ya lindi na Mtwara.
Akizungumzia kampeni hiyo alisema mkulima wa korosho sasa akipokea fedha za mauzo kupitia Benki ya NMB mbali ya huduma bora anaweza kuwa miongoni mwa washindi mbalimbali wa zawadi ambazo benki ya NMB imetenga kwa ajili ya kampeni hii.
NMB imetenga pikipiki tano kwa ajili ya wakulima ambapo kila mwisho wa wiki kutaendeshwa droo ya kutafuta mshindi atakaejinyakulia pikipiki hiyo. Droo hii itaendeshwa kwa kipindi cha wiki tano. Pia wakulima wengine watano watajinyakulia fedha taslimu kiasi cha Sh100,000 kila mmoja katika kila droo.
“Maana yake ni kwamba kila wiki tutashuhudia wakulima watano wakijishindia pesa taslimu itakayowekwa katika akaunti zao pamoja na mmoja kujishindia pikipiki”alisema Meneja wa Kanda ya Kusini.
lIi mtu ashinde zawadi hizo anatakiwa kuwa na akaunti ya Benki ya NMB, ajishughuishe na biashara katika mnyororo wa thamani ya Kilimo na apitishe mauzo yake katika Benki ya NMB.
“Tumechagua zawadi ya pikipiki ikiamini kuwa kwa kutumia pikipiki hizi wakulima watapata unafuu wa kutembelea maeneo mbalimbali walipo wateja au mashamba na urahisi wa shughuli mbalimbali”alisema Faraja .
Aidha katika uzinduzi wa kampeni hiyo droo ya kwanza ilichezeshwa ambapo Mkulima kutoka Newala, Said Likumbeya alijishindia pikipiki.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abass Ahmed aliipongeza Benki ya NMB kwa kuendeleza kampeni hii ya kuhamasisha wakulima kutumia Benki katika kupokea malipo ya mauzo ya mazao yao.
Alisema wakulima wengi wamekuwa wakikutana na maswahibu mbalimbali katika kipindi hiki hasa yanayo husiana na uhalifu sababu ya kukaa na fedha nyingi ndani mwao badala ya kuzihifadhi sehemu salama kama Benki ya NMB.
Mkuu wa mkoa alisema ni imani yake kuwa NMB itaendelea kuandaa kampeni kama hizi kwa wakulima na watu walio kwenye sekta zingine kama biashara na uvuvi.
“Wana Mtwara wenzangu kuweka fedha zako benki kwa namna moja au nyingine inakupa nidhamu nzuri ya matumizi ya fedha hivyo kukuruhusu kuiweka kwa kipindi kirefu na hata fedha hiyo kukusaidia katika nyakati ngumu au za dharura” alisema Kanai Ahmed.
Suala la kujiwekea akiba ni muhimu kwa maisha ya kila siku maana yanaibuka masuala ya dharura yatakayohitaji fedha.
Tujifunze kuweka akiba maana Akiba ni msaada mkubwa sana na namna ambavyo itakusaidia ni ya kipekee.
“Huu ndio wakati wa kuzitumia vyema akaunti zetu za NMB tunavyokwenda kuanza kufanya mauzo ya korosho zetu, tuwasihi wanunuzi wote kutulipa kwa kuweka fedha kwenye akaunti kwani ni salama sana na pia inakwenda kukuhamasisha kuweka akiba” aliongeza.
“Fedha hizi zinazowekwa kwenye akaunti ni za kwetu, kwa usalama wa fedha zetu na hata akiba ni kwa ajili yetu, lakini wao wanakupa zawadi, hili ni jambo kubwa sana” Kanai Ahmed Abbas.
Aidha Kanali Abbas aliwataka wakulima wa mkoa wa Mtwara kuendelea kuweka akiba ya kutosha ili zawadi nazo zije Mtwara.
“Kwa walio na Akaunti za NMB changamkieni fursa na wasio na akaunti, muda ndio huu kafungueni akaunti haraka sana muanze kuzitumia na mjishindie mazawadi kemkem kutoka benki ya NMB”,
Akizungumza katika tukio hio, Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda aliishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kuufungua mkoa wa Mtwara.
Awali, Meneja Mkuu wa Idara ya Kilimo katika Benki ya NMB, Wogofya Mfalamagoha, aliwakumbusha viongozi wa vyama vya ushirika kuhusu huduma za kirafiki za Benki ya NMB wakati huu, ambazo ni pamoja na mikopo ya kirafiki sana kwa kilimo kwa wakulima na vyama vya ushirika, na mkopo wa kidijitali uitwao ‘Mshiko fasta’ ambao haohitaji dhamana au kutembelea matawi yoyote.
“Tuna huduma mbalimbali zinazofaa sana kwa wakulima, kama vile mkopo rafiki wa asilimia 9 tu ya riba kwa mikopo ya kilimo na uwepo wa Mshikofasta, mkopo wa kidijitali ambao hautaki dhamana au kutembelea matawi yoyote, umekuwa na faida kubwa kwa wakulima,”alisema Wogofya.