Home LOCAL NISHATI YAONGOZA KAMATI YA BUNGE NCHINI INDIA

NISHATI YAONGOZA KAMATI YA BUNGE NCHINI INDIA

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika ziara ya kikazi nchini India,kuanzia terehe 19 hadi 24 Novemba, 2023

Wizara ya Nishati yaongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika ziara ya kikazi nchini India

Kujifunza hatua iliyopigwa na India katika matumizi ya Gesi Asilia, Nishati Safi ya Kupikia na Uzalishaji wa Umeme kutumia Makaa ya Mawe

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imewasili Jijini New Delhi, nchini India kwa ziara ya kikazi na kujifunza namna Serikali ya India ilivyopiga hatua katika matumizi ya Gesi Asilia (CNG na LNG), Nishati Safi ya Kupikia na Uzalishaji wa Umeme kwa kutumia Makaa ya Mawe.

Ziara hiyo inaongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, kwa upande wa Serikali, ambapo pamoja na mambo mengine, amesema kuwa kamati hiyo itajifunza masuala mbalimbali kuhusu Sekta ya Nishati, Ushirikiano uliopo miongoni mwa wadau pamoja na jitihada zianazofanywa na Serikali ya India katika kuongeza matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Mhe. Kapinga amesema kuwa, Ziara hiyo ya siku 7 kuanzia tarehe 19 hadi 24 Novemba, 2023 imelenga kutoa mafunzo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Sekta ya Nishati hasa katika masuala ya Nishati ya Gesi Asilia na uzalishaji wa Umeme kwa kutumia Mkaa ya Mawe.

Alifafanua kuwa Kamati inatembelea makampuni na viwanda mbalimbali, ambapo tayari imetembelea Kampuni ya Mafuta ya India (Indian Oil) inayoendesha Kiwanda cha Kujaza Gesi Asilia (Liquidfied Natural Gas LPG), kilichopo katika Mji wa Dehli.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Kilumbe Ngenda ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kuandaa na kuwezesha ziara hiyo hasa kipindi hiki ambacho nchi yetu ipo katika mipango na mikakati madhubiti ya kuipa kipaumbele sekta ya nishati hasa Gesi Asilia katika matumizi mbalimbali.

Vilevile amesema ni muda Muafaka kwa wao kufanya ziara ya kujifunza katika nchi ilizopiga hatua, ili na wao kama wawakilishi wa wananchi waweze kuongeza msukumo kwa wananchi wanaowaongoza juu ya Matumizi ya Nishati Safi na Salama ya kupikia kwa lengo la kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika azma yake ya kuwataka ifikapo mwaka 2033, asilimia 80 ya watanzania wote wawe wanatumia Nishati safi na salama kwa kupikia.

Kwa Upande wake Uongozi wa Kiwanda hicho umeieleza Kamati hiyo kuwa inafanya shughuli za Ujazaji wa Gesi kwenye Mitungi ya Kilo 5, 15 na 32 na kwa siku inasambaza gesi hiyo kwa wateja zaidi ya Milioni 5.

Vilevile Uongozi huo umeeleza kuwa, Serikali ya India imeweka juhudi katika kupunguza madhara ya kiafya yanayotokana na Matumizi ya Nishati zisizo Safi na Salama kwa kupikia kwa kutoa Ruzuku kwa familia Masikini takribani Milioni 310 na familia zenye kipato cha chini takribani Milioni 100, teknolojia ambayo imewezesha familia hizo kutumia Gesi kupikia.

Sambamba na hilo, Serikali ya India imetoa Ruzuku kwa Mawakala wa Usambazaji wa Gesi takribani Milioni 25 ili kuongeza wigo wa matumizi ya gesi kwa wananchi wa India.

Kampuni ya Mafuta ya India inamilikiwa na Serikali ya India kwa asilimia 75, mbali na kusambaza gesi kwa wateja pia inatoa elimu kwa umma kuhusu Matumizi ya Nishati Safi na Salama.

Katika ziara hiyo, Kamati imeambata na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athuman Mbuttuka, Maafisa Waandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati pamoja na Sekretarieti ya Kamati hiyo.

Previous articleSOMA HABARI MAGAZETI YA LEO ALHAMISI NOVEMBA 23-2023
Next articleTAASISI YA TOMA KUWALETA WAANDISHI WA HABARI ZA MITANDAO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here