Home LOCAL MUINGILIANO MKUBWA WA BINADAMU NA WANYAMA WATAJWA CHANZO CHA MAGONJWA

MUINGILIANO MKUBWA WA BINADAMU NA WANYAMA WATAJWA CHANZO CHA MAGONJWA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama  akizungumza wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Afya Moja lililofanyika Tarehe 03,2023 Jijini Dodoma

MUINGILIANO MKUBWA WA BINADAMU NA WANYAMA WATAJWA CHANZO CHA MAGONJWA

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Imeelezwa kuwa mwingiliano mkubwa wa shughuli za kijamii na kiuchumi, mwenendo na mifumo ya maisha na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kumekuwa na ongezeko la magonjwa yanayoibuka kutokana na mwingiliano uliopo baina ya binadamu, wanyama na mazingira.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 3, 2023 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Afya Moja ambapo amesema kuwa duniani kote takriban visa bilioni 1 vya ugonjwa na mamilioni ya vifo hutokea kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Baadhi ya Washiriki wakisikiliza Kongamano la Kitaifa la Afya Moja lililofanyika Tarehe 03, 2023 Jijini Dodoma .

Amezitaka Wizara, Idara na Taasisi za Umma, Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo kuendelea kuimarisha utekelezaji wa masuala ya usimamizi wa dharura ili kuhakikisha shughuli zote za maendeleo zinakuwa stahimilivu kwa maslahi mapana na Nchi.

“Asilimia 60 ya magonjwa ya kuambukiza yanayoibuka ambayo yanaripotiwa ulimwenguni kote ni magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Aidha, zaidi ya 75% ya vimelea vipya vya magonjwa vilivyogunduliwa katika miongo mitatu iliyopita, 30% vimetoka kwa wanyama. Changamoto hii ni kubwa na inahitaji ushirikiano wa kisekta ili kudhibiti magonjwa haya na matukio mengine yenye athari mtambuka kwa kutumia mbinu ya Afya Moja,” Amesema Mhe. Mhagama

Amesama Madhara ya maafa yanayotokana na magonjwa ya milipuko ni suala mtambuka ambalo linahusu sekta nyingi na hivyo kuhitaji juhudi za pamoja katika kuweka mikakati ya kusimamia mwenendo wake kabla hayajasambaa ili kuzuia na kuimarisha mifumo ya kuyakabili pindi milipuko inapotokea ili kupunguza madhara ya maafa,hatua hii ni muhimu ili kuwa na ufanisi katika kuthibiti magonjwa ya milipuko.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Urtaibu) Dkt. Jim Yonazi akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Afya Moja lililofanyika Tarehe 03, 2023 Jijini Dodoma.

“Niwahakikishie kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuzingatia na kusimamia Sera, Sheria na Mikakati kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisekta katika kupambana na magonjwa ya milipuko na matukio yanayoathiri binadamu, wanyama na mazingira.

Waziri Mhagama amesema sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.6 ya Mwaka 2022 inabainisha majukumu ya kutekelezwa kwa kuzingatia ushirikiano wa wadau kwa dhana ya Afya Moja. Vilevile, Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa 2022 – 2027 umeanisha umuhimu wa kutekeleza hatua za kuimarisha uwezo wa kutumia dhana ya Afya Moja kwa maafa yanayohusiana na masuala ya afya katika ngazi zote kwa ustahimilivu wa jamii.

“Dhana hii ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano baina ya sekta zinazohusika na afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwa ajili ya uratibu na usimamizi katika utendaji na kupanga mikakati ya pamoja inayolenga kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea na mazao ikiwemo madhara ya majanga yanayovuka mipaka na yanayoweza kusambaa kwa muda mfupi, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, usalama wa chakula na lishe na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,”amesema Mhagama.

Nao baadhi ya washiriki wa kongamano hilo wamesema kuwa dhana ya Afya Moja faida yake ni njia inayowaleta pamoja na sekta mbalimbali ambapo ni afya, mifugo na wanyamapori ili kukabiliana na changamoto zinazohusiana na afya.

“Upande wa kutumia Afya Moja maana yake tumefanikiwa kuhakikisha kwenye masuala yanayohusiana na milipuko ya magonjwa tunaenda kama sekta mbalimbali tunaziratibu sekta na kuzisimamia kwamba zinasaidia kutatua changamoto ya afya kwa wakati mmoja,”wamesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amefafanua kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu inawajibu wa kuratibu na kusimamia maafa yatokanayo na magonjwa ya mlipuko yanayoathiri binadamu, wanyama na mimea kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.6 ya Mwaka 2022 na Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa 2022-2027.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi pamoja na watumishi katika ofisi yake mara baada ya kufungua ufunguzi wa Kongamano la Afya Moja lililofanyika Tarehe 03, 2023 Jijini Dodoma

 

“Utekelezaji wa dhana ya Afya Moja unazingatia Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja 2022 – 2027 ambapo masuala yaliyoainishwa kutekelezwa kwa ushirikiano ni pamoja na magonjwa yanayoenea baina ya wanyama na binadamu, usalama na ulinzi wa vimelea hatarishi vya magonjwa, usalama wa chakula na lishe, usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawana hatari nyingine zinazoibuka,” Amesema Dkt. Yonazi.

Akiwasilisha taarifa kuhusu Dhana ya Afya Moja Mkurugenzi wa Dawati la Afya Moja Ofisiya Waziri Mkuu Dkt. Salum Manyata amesema ni dhana inayotumika kuweka ushirikiano baina ya sekta zinazohusika na afya ya binadamu, wanyama na mazingira, ili kuimarisha uratibu na usimamizi katika utendaji na kupanga mikakati ya pamoja inayolenga kuzuia, kujiandaa, na kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

Previous articlePRESIDENT SAMIA URGES AFRICAN COUNTRIES TO TELL THEIR OWN STORIES
Next articleBRELA: BRELA YATOA MSAADA KWA WAGONJWA OCEAN ROAD

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here