Home BUSINESS GGML YAIBUKA KAMPUNI INAYOAMINIKA ZAIDI KATIKA TUZO ZA MLAJI

GGML YAIBUKA KAMPUNI INAYOAMINIKA ZAIDI KATIKA TUZO ZA MLAJI

NA: MWANDISHI WETU

GEITA Gold Mining Limited (GGML) imeibuka kuwa kampuni inayoaminika zaidi kwenye sekta ya madini katika tuzo za mlaji (Consumer’s Choice Awards Africa) zilizotolewa mwisho mwa wiki iliyopita.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo zilizofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa GGML, Stephen Mhando alisema, “Tuzo hii ni uthibitisho wa kazi bora na muhimu tunayoifanya nchi nzima. Moja ya maadili yetu ya msingi ni kuhakikisha kuwa jamii inanufaika kutokana na uwepo wa GGML katika eneo hilo.

Alisema kampuni hiyo ambayo vipaumbele vyake vinalenga kuzingatia utu na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yake, vimeendelea kuimarisha mahusiano mazuri baina ya kampuni hiyo kupitia mpango wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

Awali, akizungumza katika hafla ya ugawaji wa tuzo hizo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alisema Serikali inatambua maendeleo ya nchi hayawezi kuletwa na Serikali pekee bali kwa kushirikiana na Sekta binafsi ambayo ni chachu ya kuleta maendeleo kwa wananchi na hivyo Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Dk. Biteko alimwakilisha Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo ya utoaji wa Tuzo za Mlaji (Consumer’s Choice Awards Africa) zilizofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 11 Novemba 2023.
Alisema kutolewa kwa tuzo hizo ni kielelezo cha mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuweka mazingira bora ya kibiashara hapa nchini.

“Hivyo wawekezaji wenye mitaji tunawakaribisha mje muwekeze Tanzania na tunawaahidi kwamba Serikali itawapa ushirikiano ili fedha mnazoweka kwenye biashara ziwape faida na pia Tanzania ifaidike kwa uwepo wa miradi husika,” alisema Dk.Biteko

Dk.Biteko alisema tuzo hizo zilizoanza mwaka 2019 zinahusisha walaji na watumiaji wa bidhaa ambao hutoa maoni na hupiga kura kuchagua kuridhishwa kwao kwa huduma wanazopata kutoka kwa watoa huduma na kueleza kuwa amefurahishwa na namna upigaji wa kura unavyofanyika kwani wale tu wanaotoa huduma bora ndio wanapata nafasi ya kupigiwa kura na kupewa tuzo.

Dk. Biteko amewapongeza waandaaji wa Tuzo hizo ambazo sasa zinafanyika kwa mwaka wa Tano. Pia amepongeza washindi wote kwa kutoa huduma bora na kuzalisha bidhaa bora.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji alisema tuzo hizo ni muhimu kwani zinakumbusha umuhimu wa wazalishaji, watoa huduma na wafanyabiashara kumjali yule anayepokea bidhaa yao au huduma yao.

Alisema tuzo hizo zimechangia katika uboreshaji wa utoaji wa huduma na bidhaa mbalimbali zinazoenda sokoni hivyo amewapongeza waandaaji wa Tuzo hizo ambazo sasa zimefikia mwaka wa Tano huku wigo wake ukiongezeka kutoka ndani ya Tanzania pekee na sasa ni Afrika kwa ujumla.

Tuzo za Consumer’s Choice Awards zimeandaliwa na kampuni ya Lavine International Agency na kampuni ya Choice Awards Africa ambapo muanzilishi wa Tuzo hizo ni Diane Laizer.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here