Home BUSINESS BRELA YATAKIWA KUZIFIKIA WILAYA ZOTE ARUSHA

BRELA YATAKIWA KUZIFIKIA WILAYA ZOTE ARUSHA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bw. Missaile Mussa ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kuhakikisha kuwa elimu ya Miliki Ubunifu inawafikia wananchi katika wilaya zote za mkoa wa Arusha ili waweze kunufaika na ubunifu wao na kufanya biashara zao bila kikwazo chochote.

Mhe. Mussa ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na maafisa kutoka BRELA waliofika kujitambulisha ofisini kwake kabla ya kuanza mafunzo kuhusu Miliki Ubunifu kwa wafanyabiashara wa Arusha Jiji, pamoja na Halmashauri za Jiji la Arusha , Halmashauri ya Wilaya ya Meru na Longido.

“Elimu ya Miliki Ubunifu inapaswa kutolewa katika Halmashauri zote zilizopo mkoani hapa, hivyo wakati mwingine mjipange kufika katika wilaya za Loliondo na Karatu ambazo hamtazifikia kwa sasa ,” amesema Mhe. Mussa.

Awali Afisa kutoka BRELA Bi. Julieth Kiwelu alimhakikishia Mhe. Mussa kuwa katika awamu hii BRELA itawafikia wafanyabiashara katika Halmashauri tatu na awamu itakayofuata wilaya zilizobaki zitafikiwa.

Bi. Kiwelu amesema lengo la Mafunzo haya ni kuhakikisha wafanyabiashara wote wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu na hatimaye kusajili Alama za Biashara na Huduma pamoja na Bunifu zao.

Mfanyabiashara ama mvumbuzi anaposajili Alama ya Biashara na Huduma pamoja na uvumbuzi wake anakuwa amelindwa kisheria, hivyo kuna manufaa yanayotokana na usajili wa Alama za Biashara na Huduma au Uvumbuzi,” amefafanua Bi. Kiwelu.

Maafisa wa BRELA wako mkoani Arusha kwa siku tano (5) kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara kuhusu Miliki Ubunifu ambayo yanajikita katika kuhamasisha usajili wa alama za biashara,
huduma pamoja na utoaji wa Hataza.

Mafunzo haya ni mwendelezo wa jitihada zinazofanywa na BRELA za kutoa elimu kwa wadau ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi.

Katika mwaka wa Fedha 2023/2024 mafunzo kama haya yamefanyika mkoani Mwanza katika Wilaya za Nyamagana, ukerewe, Ilemela na Misungwi.

Previous articleNMB, ORYX TANZANIA WAZINDUA MOTO MKALI BEI POA, KUKOPESHA GESI YA KUPIKIA
Next articleVYAMA VYA SIASA VYAONESHA USHIRIKIANO UBORESHAJI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA TABORA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here