NA: JOHN BUKUKU, ARUSHA
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itaendelea kusimamia kwa ufanisi mifumo ya miamala pamoja na malipo kwa njia ya mitandao ya simu katika kuhakikisha fedha zote zinakuwa salama.
Akizungumza katika maonesho ya Wiki ya Huduma ya Fedha yanayofanyika kwenye wanja wa Sheilh Amri. Abeid Jijini Arusha, Afisa Kitengo Cha Malipo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Bi. Joyce Njau, amesema kuwa majukumu yao ni kusimamia mifumo ili kuhakikisha malipo yote yanakuwa salama.
Bi. Njau amesema kuwa kupitia maonesho ya wiki ya huduma ya fedha watanzania wanakumbushwa kuwa BoT inaendelea kusimamia mifumo ya malipo kwa njia ya mitandao.
“Makampuni ya mitandaoni ya simu wakati wanaomba leseni kuna kipengele wanapaswa kuwa na miundombinu (Data Center) na BoT huwa tunakagua ili kuona mifumo yao inavyofanya kazi” amesema
Amefafanua kuwa mtu yoyote anayeweka fedha katika mitandao ya simu ikitokea ameacha kutumia kwa muda wa miaka mitano fedha hizo zinapelekwa BoT kwa ajili ya kuhifadhi.
“Unakuta mtu amekufa na ameacha pesa katika laini, kuna sheria namba 31 ya mitandao inayoutaka mtandao husika kama namba au akaunti imekaa kwa muda wa miaka mitano bila kutumika sheria inamtaka arudishe fedha Benki Kuu”
Amesema kuwa baada ya miaka mitano kama mtu akirudi atarudushiwa fedha zake kwa kufuata utaratibu wa kwenda katika mtandao husika kwa kujaza taarifa muhimu ambazo zinamuelekza kwenda BoT kurudishiwa fedha zake kupitia hazina.