Home BUSINESS WAKUTANA KUJADILI ITIFAKI ZINAZOSIMAMIWA NA SHIRIKA LA MILIKI UBUNIFU AFRIKA

WAKUTANA KUJADILI ITIFAKI ZINAZOSIMAMIWA NA SHIRIKA LA MILIKI UBUNIFU AFRIKA

Kamati ya Uratibu wa zoezi la kuridhiwa kwa Itifaki zinazosimamiwa na Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (African Regional Intellectual Property Organization – ARIPO), imekutana kujadili Itifaki zinazosimamiwa na Shirika hilo. Kikao hicho kilichoanza Oktoba 2, 2023 katika ukumbi wa Ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam kitahitimishwa Oktoba 4, 2023.

Katika Kikao hicho Maafisa kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (Copyright Society of Tanzania – COSOTA) pamoja na wadau mbalimbali wanajadili Itifaki zinazosimamiwa na ARIPO ili kupendekeza uwezekano wa Itifaki hizo kuridhiwa na Nchi. Itifaki hizo ni pamoja na Itifaki ya Arusha ya Ulinzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea, Itifaki ya Kampala ya Ulinzi wa Hiyari wa Hakimiliki na Hakishiriki, Itifaki ya Banjul ya Ulinzi wa Alama, Itifaki ya Madrid ya ulinzi wa Alama inayosimamiwa na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani pamoja na Itifaki ya Ulinzi wa Haki za Miliki Ubunifu Chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika ( African Continental Free Trade Area (AfCFTA).

Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Bi. Loy Mhando , akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, amesema, Itifaki hizo ambazo Nchi Ilizisaini kwa nyakati tofauti, zitaongeza wigo katika kulinda Bunifu na Hakimiliki za kazi za wabunifu ikiwa ni pamoja na kazi za sanaa, uandishi, uzalishaji, utaoji huduma, hakimiliki za aina mpya za mbegu za mimea na bunifu nyingine.

Katika Kikao cha tarehe 02 Oktoba, Itifaki ya Arusha ya Ulinzi wa Aina mpya za Mbegu za Miimea imejadiliwa ambapo Afisa Mwandamizi kutoka BRELA, Bw. Seka Kasera ameongoza mjadala huo ambapo Kamati imejadili juu ya Ulinzi wa Hakimiliki za Wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea Kikanda.

Kamati pia imepitia Itifaki ya Kampala ya Usajili wa Hiyari wa Hakimiliki na Haki Shiriki ambayo imewasilishwa na Bw. Prosper Massawe, Afisa kutoka COSOTA ambaye ameelezea namna wasanii wanavyoweza kunufaika kupitia Itifaki hiyo.

Ameelezea kuwa Itifaki hiyo itasaidia wasanii kuongeza wigo katika Umiliki wa kazi zao na pia kupunguza changamoto na kuwaongezea mapato yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here