Home LOCAL TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA SHIRIKA LA MAKAZI ALGERIA

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA SHIRIKA LA MAKAZI ALGERIA

Wajumbe wa Kikao maalum cha mabadiliko ya Shelter Afrique kikiendelea Jijini Algeria leo.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Shelter Afrique ukiwa na mazungumzo na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria leo

Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania Nchini Algeria leo

Wajumbe wafanya mazungumzo na Balozi Tanzania nchini humo

Na: Mwandishi Wetu, Algiers, Algeria

Ujumbe wa Tanzania unaohudhuria Mkutano Mkuu wa dharura wa Shirika la Makazi Afrika(Shelter Afrique) unaofanyika Jijini Algiers umekutana na Maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Algeria ili kupata uzoefu wa uendelezaji wa Miji na Makazi unaofanyika katika Taifa hilo.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika ubalozini eneo la Hydra Jijini humo, Kiongozi wa Msafara huo Bw. Deogratius Kalimenzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Miji na Vijiji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema kuwa Tanzania ni mwanachama wa Shirika hilo na lengo la kikao hicho cha dharura cha Shirika hilo ni kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ya kitaasisi ili hatimaye Shirika hilo liingie kwenye mfumo wa kuwa benki ili kuweza kubeba jukumu kubwa la kuhudumia nyumba na maendeleo ya makazi katika Afrika.

Amebaishia kuwa kikao hicho kinaenda kupanua maeneo ya kuboresha makazi ya watu na ili kufanya hivyo Shirika hilo linabidi liwe na fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.

Ameongeza kuwa hoja mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo namna ya hisa za Shirika hilo zitakavyokuwa kwa kila nchi wanachama na kushirikisha wadau wengine zikiwemo taasisi zingine. Aidha, ajenda zingine ni namna mamlaka ya kuajiri na kuanzishwa kwa Bodi ya Ushauri ya Shirika hilo itakayosimamiwa na mawaziri 6 wa nchi wanachama wanaosimamia masuala ya fedha na uchumi.

“Tanzania ina changamoto ya makazi na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 iliyojumuisha sensa ya majengo Tanzania ina majengo 14 milioni ambapo asimia 91 ni kwa ajili ya makazi. “

Kwa mujibu wa sensa hiyo ina watu milioni 61.7 na idadi hiyo inaongezeka kwa asilimia 3.2 Akasema kuwa kuna upungufu wa nyumba milioni 3.8 na kila mwaka mahitaji ya nyumba yanaongezeka kwa idadi ya nyumba 390,000 na uwezo wa taasisi ndani ya nchi wa kujenga nyumba ni asilimia 0.02 ya mahitaji ya nyumba kwa mwaka.

Amesisitiza kuwa Tanzania inahitaji kuwa na teknolojia ya ujenzi wa nyumba inayoikubalika na jamii na kuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha za kugharamia ujenzi.

Ameongeza kuwa amefurahishwa na ujenzi wa majengo ya ghorofa yaliyojengwa katika Jiji la Algiers na asema Tanzania imeanza kuweka msisitizo wa ujenzi wa majengo ya ghorofa ili kupunguza gharama za uwekaji wa miundombinu na kusambaza huduma muhimu za kijamii.

“Tanzania inahitaji Shirika hilo la nyumba Afrika ili kufungua milango ya uwekezaji katika sekta ya nyumba na makazi,” alisisitiza.

Aidha, amesema kuwa Tanzania imeshanufaika na mikopo kutoka Shelter Afrique ambapo Shirika la Nyumba la Taifa lilipata mkopo wa kujenga nyumba za gharama nafuu wa Shilingi 15bilioni.
Akauomba Ubalozi wa Tanzania Algeria kuwezesha ujumbe huo wa Tanzania kukutana na Wizara ya nyumba na Maendeleo ya Miji ya Algeria ili kufahamu namna walivyofanikiwa kujenga nyumba 40,000 kwa mwaka na kuwa na miundombinu madhubuti katika Miji mingi ya nchi hiyo.

Akijibu maombi ya ujumbe wa huo katika Mkutano huo Afisa Balozi wa Tanzania Algeria aliyemuwakilisha Balozi, Bw. Must Suleyman alisema kuwa Algeria imepiga hatua kutokana na serikali yao kuwekeza vilivyo katika ujenzi wa miji na miundombinu.

Alisema Ubalozi huo umefanya mashauriano na nchi ya Algeria na kuweka makubaliano kupitia tume ya pamoja iliyoundwa kusaidia kubadilishana mambo mbalimbali ikiwemo sekta ya nyumba, makazi na mafuta.

Wamekubali kuendelea kuishawishi nchi hiyo kusaidia Tanzania teknolojia na fedha za kufanya maendeleo ya nyumba nchini Tanzania.

Mkutano huo wa Shelter Afrique umefunguliwa leo Jijini Algeria na unahusisha nchi wanachama 45 wa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Oktoba 5 Mkutano huo unatarajia kupitisha maazimio kadhaa yatakayowezesha kulibadili Shirika hilo na kuwa Benki ya Maendeleo ya Shelter Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here