Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ilifanya mkutano wake wa 228 tarehe Fax No. 2234217
27 Oktoba 2023, kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo na mwelekeo wa uchumi. Kamati ilibaini kuwa utekelezaji wa sera ya fedha ulichangia kuwepo kwa kiasi cha kutosha cha ukwasi kwenye uchumi kwa mwezi Agosti, Septemba na Oktoba 2023. Utekelezaji wa sera ya fedha, pamoja na sera thabiti za kibajeti, na kimfumo, zimesaidia kukabiliana na shinikizo la mfumuko wa bei, kuchangia ukuaji wa shughuli za kiuchumi na uhimilivu wa sekta ya fedha nchini licha ya mtikisiko wa kiuchumi duniani. Utekelezaji wa sera ya fedha pia umesaidia kupunguza shinikizo linalotokana na ongezeko la mahitaji ya fedha za kigeni nchini.
Kamati pia, ilitathmini mwenendo wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2023 na kubaini kuwa, uchumi wa dunia bado haujaimarika licha ya ukuaji wa juu ya matarajio uliofikiwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka. Mwenendo huu unatokana na kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi nyingi duniani, migogoro ya kisiasa na ongezeko la bei za mafuta. Mfumuko wa bei umepungua kutoka viwango vilivyofikiwa mwaka 2022, licha ya kubakia juu ya malengo kwa nchi nyingi. Ili kuhakikisha mfumuko wa bei unabakia ndani ya malengo, nchi nyingi zimeendelea kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la kupunguza ukwasi.
Katika kutathmini mwenendo wa uchumi hapa nchini, Kamati ilibaini kuwa:
- Pato la Taifa kwa Tanzania Bara lilikua kwa kiwango cha kuridhisha cha asilimia 5.4 na asilimia 5.2 katika robo ya kwanza na ya pili, mtawalia na kuna matarajio ya kufikia makadirio ya ukuaji wa asilimia 5.3 kwa mwaka 2023. Kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikua kwa asilimia 6.2 katika robo ya kwanza ya 2023, na kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa asilimia 7.1 kwa mwaka 2023.
- Mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara umepungua na kufikia asilimia 3.3 mwezi Septemba 2023, kutoka asilimia 3.6 mwezi Juni 2023, ukichangiwa na kupungua kwa bei za vyakula. Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 7.5 ukilinganisha na asilimia 6.5 mwezi June 2023,
1 ukichangiwa na ongezeko la bei za vyakula. Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5, licha ya ongezeko la bei za mafuta hivi karibuni.
iii. Ukuaji wa ujazi wa fedha (M3) ulikuwa wastani wa asilimia 17.7 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2023/24 juu ya makadirio ya ukuaji wa asilimia 10.1 kwa mwaka unaoishia Desemba 2023. Mwenendo huu ulitokana na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ambao ulifikia takriban asilimia 22 kwa kipindi cha mwezi Julai na Agosti na asilimia 19.5 mwezi Septemba 2023, ukilinganisha na
makadirio ya ukuaji wa asilimia 16.4 kwa mwezi Desemba 2023. Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulitokana na ongezeko la mahitaji ya mikopo mipya kufuatia kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini, ukichagizwa na utekelezaji thabiti wa sera ya fedha. Aidha, shughuli za kilimo zimeendelea kunufaika kwa kiwango kikubwa na ongezeko la kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.
- Ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa Tanzania Bara ulikuwa wa kuridhisha ambapo makusanyo yalifikia asilimia 96.2 ya lengo katika robo ya kwanza ya mwaka 2023/24. Kwa upande wa Zanzibar, ukusanyaji wa mapato ulivuka lengo kwa asilimia 1.7. Matumizi ya Serikali yameendelea kufanyika kulingana na mapato.
- Nakisi ya urari wa biashara, huduma na uhamisho mali nje ya nchi imeendelea kuwa kubwa kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa katika soko la dunia. Hata hivyo nakisi hii ilipungua kufikia dola milioni 3,652.6 kwa mwaka unaoishia Septemba 2023, kutoka dola milioni 4,728.1 kwa mwaka ulioishia Septemba 2022, kutokana na ongezeko la mapato yanayotokana na shughuli za utalii.
Nakisi hii inatarajiwa kupungua zaidi kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara nje ya nchi. Kwa upande wa Zanzibar nakisi ya urari wa biashara, huduma na uhamisho mali nje ya nchi ilifikia dola za Marekani milioni 417.1 ukilinganisha na dola za marekani milioni 344.4, kutokana na ongezeko la gharama za uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.
- Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kubaki katika viwango vya kuridhisha vya takribani dola za Marekani bilioni 5 katika kipindi cha mwezi Julai mpaka Oktoba 2023, kiwango kinachotosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na
2 huduma nje ya nchi, juu ya viwango vya nchi na jumuiya ya Afrika Mashariki vya miezi 4 na 4.5 mtawalia.
vii. Sekta ya benki iliendelea kuwa na mtaji, ukwasi wa kutosha na inayotengeneza faida. Ubora wa rasilimali umeendelea kuimarika, kufuatia kupungua kwa viwango vya mikopo chechefu kufikia asilimia 5.2 mwezi Septemba 2023, kutoka asilimia 7.3 mwezi Septemba 2022. Kupungua kwa viwango vya mikopo chechefu kunategemewa kuongeza chachu ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.
Kamati pia, ilibaini uhaba wa fedha za kigeni ulioonekana hivi karibuni nchini umeendelea kupungua kufuatia ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara nje ya nchi. Uuzaji wa fedha za kigeni uliofanywa na Benki Kuu kwa lengo la kukabiliana na ongezeko la mikopo inayotokana na uagizaji wa bidhaa nje ya nchi pia umepunguza changamoto hii. Hali ya upatikanaji wa fedha za kigeni inatarajiwa kuendelea kuimarika kutokana na matarajio ya mapato yanayotokana na shughuli za utalii, uuzaji wa madini na mazao ya biashara, pamoja na hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu na Serikali katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa fedha za kigeni.
Kwa kuzingatia mwenendo wa uchumi wa dunia na wa hapa nchini, Kamati ya Sera ya Fedha iliamua kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kasi ya ongezeko la ukwasi katika uchumi. Sera ya fedha itaendelea kutekelezwa sambamba na sera za kibajeti na kimuundo ili kufikia malengo ya kiuchumi. Aidha, utekelezaji wa Sera ya Fedha unalenga kuhakikisha malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya Extended Credit Facility (ECF) kwa robo inayoishia Desemba 2023 yanafikiwa.
GAVANA
BENKI KUU YA TANZANIA