Home LOCAL MSD KANDA YA IRINGA YAKABIDHI VIFAA TIBA KITUO CHA AFYA KIFANYA

MSD KANDA YA IRINGA YAKABIDHI VIFAA TIBA KITUO CHA AFYA KIFANYA

MGANGA Mfawidhi wa halmashauri ya Mji wa Njombe Dk.Jabir Juma wa pili kushoto mwenye tisheti ya blue akionyesha vifaa tiba vilivyotolewa na Bohari ya Dawa (MSD) na kufungwa katika kituo cha Kifanya katika halmashauri hiyo wa pili kulia ni Meneja wa MSD Iringa Robert Lugembe, Diwani wa Kata ya Kifanya Nolasco Mtewele (kulia) na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Weston Mtega (Na Mpiga picha wetu

Na: Mariam Mziwanda: NA MWANDISHI WETU.

BOHARI ya Dawa (MSD) Kanda ya Iringa imekabidhi vifaa tiba katika kituo cha afya cha Kifanya Halmashauri ya Mji wa Njombe mkoani humo vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 200.

Kituo hicho cha afya ni kati ya vituo vipya vilivyojengwa na serikali hivi karibuni lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wananchi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki Meneja wa MSD Kanda ya Iringa Robert Lugembe, alisema hatua hiyo ni katika kuunga mkono juhudi za serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya.

Alisema MSD imehakikisha kabla ya kituo hicho kuanza kazi miundombinu yake inaendana na thamani ya huduma watakazopewa wananchi.

“Huduma ili ziwe bora ni lazima kuwapo kwa vifaa vya kisasa na dawa zote muhimu nasi tumehakikisha vinakuwepo tumekabidhi dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 200 na vingine vinakuja,”alisema.

Alisema, hatua hiyo imefikiwa kutokana na ushirikiano uliopo kati ya bohari na viongozi wa halmashauri ambapo mara baada ya kukamilika kwa ujenzi mahitaji yote muhimu yamepatikana.

Lugembe, alitaja dawa na vifaa tiba hivyo kuwa ni dawa zote muhimu na nyingine, vifaa vya maabara, upasuaji , vya kutakasa vyombo, vitand a vya kujifungulia na vifaa vya kupashia watoto joto maalumu kwa ajili ya watoto njiti.

“Vifaa vingine ni vya CEmONC, gari ya kubebea wagonjwa na vifaa vya chumba cha kuhidhia maiti,”alisema.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Dk. Jabir Juma, alisema ujenzi wa kituo hicho umegharimu zaidi ya sh. milioni 550 ikiwa ni fedha za ndani za halmashauri, fedha za Rais na nguvu ya wananchi.

“Kituo hicho kilianza ujenzi mwaka 2018 kwa nguvu za wananchi na uongozi wa halmshauri hiyo na wakati wa ziara ya Rais Dk.Samia hapa Njombe alikuta ujenzi huu na kuamua kutoa fedha zake mfukoni sh. milioni 10 kuunga mkono.

Dk.Juma alisisitiza kuwa, miongoni mwa majengo hayo ya kisasa ni jengo la mama na mtoto, upasuaji, wodi ya kina mama, maabara na jengo la kuhifadhia maiti lenye jokofu kubwa linaloweza kuhifadhi miili sita kwa wakati moja.

Alitumia fursa hiyo kushukuru MSD kwa kuwa hatua hiyo ilikuwa inahitaji uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kisasa na vyote vimepatikana kwa wakati hivyo, anatoa rai kwa wananchi kutunza miundombinu hiyo na watoa huduma kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo na maadili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here