Home LOCAL DODOMA YAVUKA LENGO UKUSANYAJI DAMU

DODOMA YAVUKA LENGO UKUSANYAJI DAMU

Na: Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Timu ya Afya ya Mkoa wa Dodoma imepongezwa kwa kuendelea kufanya vizuri katika suala la uchangiaji damu hadi kuvuka lengo la asilimia 100 lililowekwa na kufikia asilimia 110 kwa sasa.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bi. Ziada Sellah ametoa takwimu hizo leo Oktoba 03, 2023 jijini Dodoma katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete linapofanyika zoezi la uchangiaji damu ikiwa ni moja ya tukio lililoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuelekea Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakaofanyika jijini humo Oktoba 05, 2023.

Bi. Ziada amesema kuwa, suala la uchangiaji damu ni la muhimu na msingi kwani ni muhimu kuhakikisha damu na mazao ya damu yanakuwepo kwa wakati wote katika Vituo vya Afya kwani kunaweza kuwa na wataalam wakafanya kila kitu lakini kama hakuna damu msaada hautofanya kitu chochote.

“Nawashukuru Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuona kuwa kuchangia damu ni jambo la msingi, hali ya uhitaji wa damu ni kubwa hasa kwa mikoa yenye idadi kubwa ya watu na tunatamani angalau kila mkoa uwe na asilimia 85 mpaka 90, tunaipongeza Timu ya Afya ya Mkoa wa Dodoma kwa kuvuka lengo lililowekwa, nawasihi Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa zoezi la uchangiaji damu lisiwe kwenye Jukwaa hili tu bali muendelee kulifanya mara kwa mara kwani damu lazima itolewe na wananchi wenyewe,” alisema Bi. Ziada.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amewakaribisha wananchi kuchangia damu ili kuwa na damu ya kutosha katika ghala za kutunzia damu kwa ajili ya kusaidia wenye uhitaji wakiwemo wagonjwa waliopata ajali, wajawazito na watoto wenye upungufu wa damu.

Aidha, amesisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu hivyo, ambapo kwa Mkoa wa Dodoma mahali pa kuchangia damu ni Kituo cha Damu Salama cha Kanda ya Kati, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma pamoja na Kituo cha Afya Makole. 

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bibi Mwantumu Mahiza amewashukuru wajumbe wa Mashirika hayo waliojumuika mkoani Dodoma kwa ajili ya Jukwaa la Mwaka la Mashirika hayo. Pia amewashukuru kwa kurudisha kwa jamii katika njia za kijamii zaidi ikiwemo kupanda miti takriban 300, kuchangia damu na kuona watoto yatima na wenye mazingira magumu.

“Kuchangia damu ni sadaka kubwa, hakuna kiwanda cha damu wala biashara ya damu lakini unapotoa damu yako umetoa damu kwa ajili ya kumsaidia mwanadamu mwenzio. Natoa wito kwa wajumbe wa mkutano wa mwaka huu na wananchi wote ambao wana sifa za kuchangia damu waweze kufanya hivyo,” amemalizia Mwenyekiti Mwantumu Mahiza.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here