Home LOCAL WAZAZI, MC, DJs WAPIGWA MARUFUKU KUSHIRIKISHA WATOTO SHUGHULI ZA USIKU

WAZAZI, MC, DJs WAPIGWA MARUFUKU KUSHIRIKISHA WATOTO SHUGHULI ZA USIKU

Na: WMJJWM

Wamiliki wa kumbi za starehe na Washereheshaji(MC) nchini, wametakiwa kuzingatia Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 ili kuwaepusha watoto na wimbi la mmomonyoko wa maadili.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amekutana na wadau hao  kufuatia kushamiri kwa vitendo vya kusambaza maudhui yanayohusisha watoto wakicheza muziki kwenye kumbi za starehe.

Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kuwa washehereshaji na wamiliki wa kumbi za starehe, wapiga muziki (DJs) na Wazazi wana nafasi kubwa katika kumlinda Mtoto ili kudhibiti mmomonyoko wa maadili dhidi ya watoto kupitia Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 kifungu cha 158 cha Katazo la Jumla.

“Pamoja na juhudi zinazofanywa na Wizara kwa kushirikiana na Wadau, bado baadhi ya familia na jamii wakiwemo wazazi na walezi hawatimizi wajibu wao kwa ufanisi kwenye malezi na makuzi stahiki ya watoto. Baadhi ya Watoto wanatumiwa kwenye shughuli ambazo zinaathiri malezi na makuzi yao ambapo ni kinyume na Sheria zinazomlinda Mtoto. Matendo hayo yasipodhibitiwa yatachochea mmomonyoko wa maadili na kuwaweka watoto katika hatari ya kufanyiwa ukatili na kujikatili wao wenyewe.” Amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima

Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii nchini kote kushirikiana na Wadau wa Maendeleo na vyombo vya habari, polisi jamii na madawati ya jinsia ya wanawake na watoto ya Jeshi la Polisi kutekeleza mpango wa elimu kwa jamii kuhusu Sheria ya Mtoto.

Ametumia nafasi hiyo pia kumuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuunda Kamati mtambuka na kuipa jukumu la kuja na mpango wa haraka, wa muda mfupi na mrefu wa kudhibiti uvunjifu wa Sheria ya Mtoto na Sheria nyingine za nchi zinazohusika na kutunza maadili.

“Natoa siku 21 nipokee yatokanayo na kazi ya Kamati hii ili nitoe mrejesho kwa jamii na kuandaa mjadala wa wazi ili jamii nayo itoe maoni yajumuishwe kwenye kazi ya Kamati kwa ajili ya umiliki wa pamoja kama jamii.” ameagiza Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa Kedmon Mapana ametoa wito kwa wadau wa sanaa kusoma na kuzingatia kanuni za Baraza hilo kwani zimefafanua vizuri namna ya kuwalinda watoto dhidi ya maudhui katika kazi zao za sanaa.

Naye Mwenyekiti wa Washereheshaji MC Boaz Mwakajumba amesema changamoto ni wazazi na walezi kutumia watoto kwenye kumbi za starehe bila kujali kuwa nyimbo nyingi zinazotungwa sasa zipo kinyume na maadili kwa sababu hazihaririwi kabla ya kusambazwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here