Home BUSINESS UFANISI KATIKA UENDESHAJI UMEWEZESHA UKUAJI WA MTAJI-NIC

UFANISI KATIKA UENDESHAJI UMEWEZESHA UKUAJI WA MTAJI-NIC

Na: Beatrice Sanga-MAELEZO

Kampuni ya Taifa ya Bima (NIC) imesema itandelea kuongeza ufanisi wake katika utoaji wa huduma na kuchangia katika mfuko wa hazina kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kufanywa ambayo yameongeza tija katika utendaji kazi wa Kampuni hiyo.

Hayo yameelezwa Septemba 11, 2023 na Dkt. Elirehema Doriye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo wakati akiwasilisha ripoti ya mafanikio ya NIC kutoka mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 katika Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, na wahariri wa Vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam ambapo amesema miongoni mwa mabadiliko yaliyofanywa na kampuni hiyo ni pamoja na kuwekeza katika rasilimali watu, wenye sifa stahiki, weledi na wabunifu.

Aidha, mabadiliko mengine ni kuanzisha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano, uwekezaji katika Mifumo ya TEHAMA kwa zaidi ya asilimia 90 na kuwa na Mtazamo na mawazo ya kibiashara yanayomuweka mteja mbele katika kazi zao, ambapo amebainisha kuwa mabadiliko hayo yamechangia kuongeza mapato na gawio kwa serikali na Kampuni na yameimarisha utoaji huduma kwa wateja.

“Kutokana na kuchukua hatua nilizozitaja, tumeweza kuondoa hasara kwa kuongeza mapato kutoka Sh. bilioni 76.45 mwaka 2019/20 hadi Sh. bilioni 103.94 kwa mwaka 2021/22, ongezeko hili ni sawa na asilimia 17.98 kwa mwaka, usimamizi madhubuti wa matumizi pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi kumeongeza ufanisi na kuondoa matumizi yasiyo na tija jambo lililoshusha gharama za uendeshaji na kuongeza faida.” Amefafanua Dkt. Doriye.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa Kampuni hiyo imefanikiwa kulipa madeni mbalimbali katika kipindi cha miaka mitatu ambapo madai ya ndani ya bima za wateja yaliyolipwa hadi kufikia Juni 2022, ni jumla ya Shilingi bilioni 33.79 kwa bima za Maisha na Shilingi bilioni 40.18 kwa bima za mali na ajali, aidha imefanikiwa kulipa gawio serikalini ambapo kwa mwaka ulioishia Juni, 2022 NIC ilitoa gawio la Shilingi bilioni 2.0 kwa Serikali ikilinganishwa na gawio la kiasi cha Shilingi bilioni 1.5 lililotolewa mwaka ulioishia Juni 2021.

“Tumeweza kulipa kodi ya mapato Serikalini kutokana na faida inayopatikana ambapo ulipaji huo umeongezeka kutoka Shilingi billioni 11.86 mwaka 2019/20 hadi Shilingi bilioni 15.14 mwaka 2021/22 sawa na wastani wa asilimia 13.80 kwa mwaka, aidha faida ghafi imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 33.65 mwaka 2019/20 hadi Shilingi bilioni 63.21 mwaka 2021/22 sawa na asilimia 43.91 kwa mwaka, lakini pia tumeweza kupata malimbikizo ya faida ya Shilingi bilioni 45.74 kufikia Juni, 2022 kutoka kiasi cha malimbikizo ya hasara ya shilingi bilioni 19.31.” Ameongeza Dkt. Doriye.

Mbali na mafanikio hayo, Dkt. Doriye amebainisha kuwa thamani ya mali za Kampuni hiyo imekua kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, kutoka mali zenye thamani ya Shilingi bilioni 350.36 mwaka 2019/20 hadi kufikia mali zenye thamani ya Shilingi bilioni 423.99 mwaka 2022, ukuaji huo ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 10.51 kwa mwaka.

“Ufanisi katika uendeshaji, umewezesha ukuaji wa Mtaji wa wanahisa kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 72.16 mwaka 2019/20 hadi Shilingi bilioni 217.07 mwaka 2021/22, ukuaji huu wa mtaji ni sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 100.40 kwa mwaka.” Ameeleza

Kampuni hiyo imesema ili kuendelea kufanya vyema katika kuwatumikia watanzania na kuwashawishi wajiunge na huduma za bima za kampuni hiyo, itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya bima katika kuelimisha kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

NIC Insurance ni kampuni inayomilikiwa na Serikali kwa 100%, ikiwa na dhamana ya kufanya biashara ya bima za mali na ajali pamoja na bima za Maisha, kati ya kampuni zaidi ya 30 zilizopo kwenye soko la bima Tanzania, NIC insurance imeweza kumudu ushindani kwa kufanya vizuri baada ya maboresho mbalimbali yaliyofanyika tangu mwaka 2019.

Previous articleNIC YAFANYA MAGEUZI MAKUBWA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITATU
Next articleNAIBU WAZIRI MKUU AONGOZA KIKAO KUJADILI UPATIKANAJI WA PETROL
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here