Home LOCAL SERIKALI KUTUMIA MIEZI 18 KUMALIZA ADHA YA UMEME MASASI

SERIKALI KUTUMIA MIEZI 18 KUMALIZA ADHA YA UMEME MASASI

Na: Immaculate Makilika – MAELEZO

Serikali imeendelea na jitihada zake za kutatua adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Mkoa wa Mtwara ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akizungumza na wananchi leo katika Uwanja wa Boma uliopo Wilaya ya Masasi, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kuhusu adha hiyo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, tayari Serikali imeanza kutatua adha hiyo na inahitaji muda ili kukamilisha.

Mhe. Rais Samia ametaja baadhi ya jitihada za Serikali “Mkandarasi yuko kazini ili kuinganisha Masasi na Gridi ya Taifa, tupeni muda baada ya miezi 18 umeme wa uhakika utafika”.

Aidha, amefafanua kuwa Serikali imejipanga kutumia Mto Ruvuma na vyanzo vingine vya maji ili kupunguza adha ya maji kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara.

Pia, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono jitihada za Serikali ikiwa ni pamoja na kufanyakazi kwa bidii. “Wakulima waanze kuongeza mashamba, kulima zaidi ili kupata mazao zaidi na kupata fedha zaidi”, ameeleza Mhe. Rais Samia.

Naye, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi trilioni 1.5 kwa vijiji 4,071 na kuwa vijiji vyote vitapata umeme ifikapo Desemba, 2023.

“Kwa Mkoa wa Mtwara, ikiwemo Masasi umetupatia fedha shilingi bilioni 98 na tayari tumeshapeleka umeme kwenye vijiji vyote vya mkoa huu ikiwemo Masasi kwenye Majimbo ya Lindi, Ndanda na Masasi Mjini”, ameeleza Mhe. Judith.

Aidha, ameongeza “Mhe. Rais ulituelekeza tuhakikishe tunapeleka umeme kwa vitongoji vyote ambavyo vimebakia Tanzania hii, vitongoji 36,036. Mwaka huu wa fedha umetupatia bilioni 348 tuanze kupeleka umeme kwenye vitongoji. Kwa Wilaya ya Masasi peke yake, Mhe. Rais umetupatia bilioni 22 na tunaenda kupeleka umeme kwenye vitongoji 167 vya Wilaya ya Masasi”.

Aidha, Mhe Rais amemaliza ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na leo anatarajiwa kuwasili mkoani Lindi kwa ajili ya kuanza ziara yake kesho.

Previous articleSOMA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI SEPTEMBA 17-2023
Next articleGST YATAKIWA KUWA KINARA WA TAARIFA ZA MADINI NA HUDUMA BORA ZA MAABARA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here