Home BUSINESS MSD: UPATIKANAJI WA DAWA NCHINI UMEIMARIKA 

MSD: UPATIKANAJI WA DAWA NCHINI UMEIMARIKA 

Na: Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Mavere Tukai amesema kuwa upatikanaji wa dawa nchini umefikia asilimia 81 mwezi Juni 2023 kutoka asilimia 57 mwezi Juni 2022 jambo ambalo limechangia kurahisisha utoaji huduma nchini.

Ameyasema hayo leo Septemba 27, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mavere amesema kuwa upatikanaji wa bidhaa za afya nchini umeendelea kuimarika siku baada ya siku kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Rais Samia umechangia upatikanaji wa bidhaa za afya kutoka asilimia 51 mwezi Juni 2022 hadi kufikia asilimia 64 Juni 2023,” amesema Mavere.

Ameongeza kuwa MSD imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi katika kufanikisha usambazaji dawa ambapo ina majukumu manne ikiwemo uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji.

“Uzalishaji unafanyika kupitia viwanda vyetu ikiwemo kiwanda cha Keko ambacho tunakimiliki kwa asilimia 70 na Serikali huku sekta binafsi ikimiliki asilimia 30” amesema.

Amesema, pia wana jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa uhakika katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na wamekuwa wakitekeleza hilo kwa ufanisi mkubwa.

Mkurugenzi Mkuu huyo amefafanua kuwa,MSD imekuwa ikifanya usambazaji wa bidhaa za afya moja kwa moja kwenye vituo.

“Usambazaji unafanyika kila baada ya miezi miwili tukiwa na magari zaidi ya 185 na makabidhiano yanafanyika kwa mfumo wa PoD (kupitia TEHAMA),” amebainisha.

Amesema, kupitia kanda zake 10 ambazo zinajumuisha mikoa ya Dar es Salaam,Tanga, Kilimanjaro, Iringa, Mbeya, Mwanza, Tabora,Kagera,Mtwara na Dodoma wanahudumia zaidi ya vituo 7,600 vya afya.

Vilevile amesema, fedha iliyopokelewa mwaka wa fedha 2022/23 ni shilingi bilioni 190.3 ikilinganishwa na shilingi bilioni 134.9 mwaka wa fedha 2021/22, sawa na asilimia 95.

Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa Ununuzi na Usambazaji wa vifaa vya huduma kwa wajawazito wanaopata uzazi pingamizi wakati wa kujifungua (CEmONC) anasema, awamu za utekelezaji ni tano.

“Na idadi ya vituo vya kutolea huduma vinavyopelekewa vifaa ni 284, jumla ya vifaa vilivyopangwa kusambazwa ni 345 na idadi ya vifaa vilivyosambazwa hadi kufikia Juni 2023 ni 299, sawa na asilimia 87,” amefafanua Mkurugenzi Mkuu huyo.

Ameongeza kuwa,thamani ya vifaa vinavyotarajia kusambazwa ni shilingi bilioni 99.7 ambapo thamani ya vifaa vilivyosambazwa ni shilingi bilioni 79.4 ikiwa ni sawa na asilimia 80 za utekelezaji.

Kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Uviko-19, Mkurugenzi Mkuu huyo wa MSD amesema, unahusu hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma za afya.

Amesema, hospitali za rufaa za mikoa ambayo MSD imetekeleza ni Kigoma, Kagera, Lindi, Katavi na Lugalo.

Tukai amesema, thamani ya vifaa vilivyotarajia kusambazwa ni shilingi bilioni 17.17 huku thamani ya vifaa vilivyosambazwa ikiwa ni shilingi bilioni 17.62 sawa na asilimia 102 za utekelezaji.

Pia amesema, ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani umeongezeka kutoka shil bililioni 14.1 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia shilingi bilioni 39.77

Aidha, amesema wamejipanga kutoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi hususani zile ambazo zinakidhi mahitaji na viwango vya ubora, hivyo kutegemea wazalishaji wa ndani.

“Na tumefanikiwa kuongeza idadi ya mikataba ya muda mrefu kutoka mikataba 100 yenye bidhaa za afya 711 kwa mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia mikataba 233 yenye bidhaa 2,209 kwa mwaka wa fedha 2022/23,” amefafanua Tukai.

MSD ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya, iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Sheria ya Bohari ya Dawa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2021.

Previous articleYASEMAVYO MAGAZETI YA LEO JUMATANO SEPTEMBA 27-2023
Next articleNAIBU WAZIRI MWANAIDI AKABIDHI MIPIRA YA MAJI MPAPA ZANZIBAR NA. MWANDISHI WETU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here