*Taasisi ziko tayari kushiriki, Rais Samia Suluhu Hassan Mgeni Rasmi
Na: Beatrice Sanga MAELEZO
Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema itahakikisha inasimamia mabadiliko na mageuzi mbalimbali katika Taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala za serikali pamoja na Kampuni na Taasisi ambazo zina ushirikiano na serikali ili kuhakikisha kuwa shughuli za uchumi na maendeleo ya Taifa na wananchi kwa ujumla zinakwenda kasi na kwa ufanisi zaidi.
Hayo yamesemwa August 13, 2023 na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea juu ya Kikao Kazi kiliachoandaliwa na Ofisi hiyo kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi (CEOs Forum) ambacho kitafanyika kuanzia August 19 hadi 21, Jijini Arusha katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kitakachowakutanisha Wenyeviti na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali na ili kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya mifumo, Sheria na kutoa mwelekeo mpya wa utendaji kazi wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili.
Mchechu amesema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika Kikao Kazi hicho ambacho mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ni pamoja na kukumbushana majukumu ya kila mmoja katika Taasisi hizo, Kujengeana uwezo kiutawala, na Teknolojia, Maboresho ya usimamizi wa Taasisi na vigezo vya utendaji kazi, Kupitia na kujadili Dira ya Maendeleo ya Taifa, kujadili changamoto za kiutendaji katika Taasisi hizo na mkakati wa kuzitatua katika Taasisi pamoja na mafunzo mbalimbali ya uongozi ili kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hizo.
“Tutakuwa na utambuzi wa baadhi ya Taasisi ambazo zimefanya vizuri, kutakuwa na utambuzi na zawadi ambazo shughuli itafanywa na Rais Samia, tumeweka utambuzi huo katika vipengele vinne, kigezo cha kwanza Taasisi zinazochangia gawio, pili, Taasisi ambazo serikali ina hisa chache ambazo zimechangia gawio kubwa serikali, lakini pia Taasisi zisizo za kibiashara, kipengele cha Taasisi zilizozalisha faida nyingi, na kipengele cha kampuni zilizobadilika zaidi kiutendaji (a most transformed company) maana kuna kampuni tulikuwa tunatamani tuzifute kabisa lakini kwa sasa zimebadilika sana, tutaenda kuzitambua na hii ni katika kuleta ushindani ndani ya Taasisi zetu, kuleta uwazi,” amesema Mchechu
Mchechu amesema katika Kikao Kazi hicho Ofisi ya Msajili imejizatiti kuhakikisha inasimamia R4 za Rais Samia ambazo ni Maridhiano (Reconciliation), Mabadiliko (Reforms) Ustahimilivu (Resilience) pamoja na Kujenga Upya (Rebuilding) ili kuhakikisha kuwa Taasisi, Wakala na Mashirika yanabadilisha mtazamo wake kiutendaji na katika uzalishaji mali, aidha amesema Kikao kazi hicho kitajadili namna ya kuboresha uhuru wa Taasisi hizo ili ziwe na ufanisi katika kusimamia rasilimali za nchi kwa maslahi ya watu wote.
“Baadhi ya Taasisi tutaangalia sheria zao ambazo labda zimepitwa na wakati zinatakiwa ziboreshwe, tutaenda kuimarisha namna ya kupata viongozi wa Taasisi hizo ili kuwa na viongozi wenye uwezo na utalaam kuzisimamia hizo Taasisi, namna ya kuchaguliwa kwa bodi za Wakurugenzi, tutakuwa tunaajiri kwa kuangalia changamoto ambazo Taasisi zake zinapitia.” amesema Mchechu.
Kwa upande wake Latifa Khamis Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) amesema kuwa kikao kazi hicho kitasaidia kupunguza milumbano mbalimbali ambayo imekuwa kitokea katika Taasisi mbalimbali na hivyo itaongeza utendaji kazi na ufanisi.
“Jukwaa letu hili malengo yake makubwa ni kurahisisha mawasiliano baina yetu ili kufanya utekelezaji wa majukumu yetu uwe rahisi, badala ya kuhangaika kumtafuta mwenzako kwa njia mbalimbali, lakini jukwaa letu litatusaidia kukusanyika pamoja ili tuweze kusaidiana katika kufanikisha utekelezaji wa malengo yetu.”