Home LOCAL WATANZANIA WAPEWA WITO KUWAENZI WAASISI WA TAIFA

WATANZANIA WAPEWA WITO KUWAENZI WAASISI WA TAIFA

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka akiwa ameshika kitabu ‘LONG WALK to FREEDOM’ kilichoandikwa na Nelson Mandela, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, ambacho ndani yake kimemuelezea John Mwakangale katika Banda la Kumbukumbu za John Mwakangale, kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane, jioni Mbeya.

Sarafina Mwakangale (kushoto), mmoja wa wajukuu wa John Mwakangale, akiwaelezea jambo wananchi waliofika kwenye Banda la John Mwakangale, kuhusu historia ya uwanja huo, kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane, jijini Mbeya.

Mwandishi Wetu

WATANZANIA wamepewa wito wa kuwaenzi waasisi wa taifa, waliokuwa mstari wa mbele kwenye harakati za ukombozi wa Tanganyika, kwa kuwa wazalendo na wenye kufuata maadili, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Stephen Mwakangale, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Banda la Kumbukumbu ya John Mwakangale, katika Maonesho ya Kitaifa Nanenane 2023 yanayofanyika jijini Mbeya, ndani ya viwanja vya John Mwakangale.

Stephen ambaye ni mtoto wa kwanza wa John Mwakangale, alisema baba yake ni miongoni mwa wanasiasa waasisi wa iliyokuwa Tanganyika African National Union (TANU), aliyeungana na Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania, katika kulipambania taifa.

“John Mwakangale na Mwalimu Nyerere walikuwa karibu sana. Kuna wakati Mwalimu alipokuwa akisoma Scotland alikutana na baba yangu ambaye naye alikuwa masomoni Uingereza, walikutana huko na kukubaliana kuja kuendeleza harakati za TANU,” alisema Stephen, akiongeza.

“Wakati tunapata Uhuru mwaka 1961 baba (John Mwakangale) alikuwa Mbunge hata hivyo Desemba mwaka 1962, Mwalimu Nyerere alimteua Mwakangale kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati huo Mbeya ikiitwa Mkoa wa Southern Highlands, ikijumuisha mikoa ya sasa Songwe, Njombe, Iringa, Rukwa.”

Alisema lengo la kuonesha kumbukumbu za John Mwakangale, kwenye maonesho hayo ni kuelezea historia ya Mwakangale tangu harakati za ukombozi wa Tanganyika chini ya TANU, Uhuru hadi Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Lengo la kuonesha kumbukumbu za John Mwakangale, ni kuhamasisha na kuielimisha jamii mazuri ambayo yalifanywa na waasisi wa taifa letu, kwa kutambua mchango wao kabla na baada ya uhuru. Mchango wao kwenye kilimo, siasa na uchumi unapaswa kukumbukwa kizazi hiki a kijacho.

“Ametambuliwa na viongozi tofauti maarafu. Nelson Mandela, kwenye kitabu chake kiitwacho ‘LONG WALK to FREEDOM’ amemuelezea John Mwakangale, na namna alivyompokea mkoani Mbeya mwaka 1962, kabla ya Mandela kwenda Addis Ababa, Ethiopia kushiriki mkutano wa Muungano wa Ukombozi Kusini na Mashariki mwa Afrika (PAFMECA),” alisema Stephen.

Alisema kwamba kabla ya uhuru, baba yake alikuwa mwajiriwa na mwanataaluma katika mifugo yaani daktari wa mifugo ilikuwa fani yake na kisha baadae aliamua kuacha utumishi wa umma na kujikita kwenye siasa na mwaka 1956 na alijiunga na TANU, akishika nafasi ya Katibu wa Mkoa.

“TANU ilipozaliwa kulikuwa na wakereketwa wengi kisiasa akiwamo baba, Nyerere, Joseph Nyerere (mdogo wa mwalimu Nyerere), Kissoky na wengine wengi, ambao walijikita katika ukombozi hata kwa za Kusini barani Afrika,” alisema Stephen.

Alisema kuwa PAFMECA, John Mwakangale, alishiriki harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na TANU ilipoasisiwa alichaguliwa na kuonyesha mchango mkubwa kisiasa na harakati hizo ilimfanya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) mwaka 1957.

Maonyesho ya Nanenane 2023 yanafanyika kitaifa jijini Mbeya, kwenye viwanja vya John Mwakangale, yamezinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni; Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here