Home BUSINESS WAKULIMA WAANIKA FAIDA MATUMIZI MFUMO T-KAKIKI, WAITA WENZAO KUJISAJILI

WAKULIMA WAANIKA FAIDA MATUMIZI MFUMO T-KAKIKI, WAITA WENZAO KUJISAJILI

Mkurugenzi wa Kampuni ya Quincewood Group Limited iliyobuni mifumo ya kiteknolojia ya  T-Hakiki na Wakala digital, Fatma Fernandes (kulia) akimkabidhi mkulima Justin Kitarima zawadi ambaye ni mmoja wa wakulima waliohudhuria mafunzo ya namna ya kutumia mifumo hiyo ya kiteknolojia katika kuwasaidia wakulima kuhakiki pembejeo zao ikiwamo mbegu na kuthibiti matumizi ya mbegu feki na kupata taarifa za afisa ugani katika maeneo yao na kuwawezesha kupata soko la mazao baada ya kuzalisha.
Na Mwandishi Wetu, Mbeya

WAKULIMA wa mikoa ya Nyanda za Juu wametoa wito kwa wakulima wenzao wa mazao mbalimbali kujisajili na mfumo wa kuhakiki mbegu kiteknolojia T-HAKIKI pamoja na Wakala Digital ili kuondokana na kilio cha matumizi ya mbegu feki. 

T-Hakiki na Wakala digital ni mifumo ya kiteknolojia iliyobuniwa na kampuni ya Quincewood Group Limited kuwasaidia wakulima kuhakiki pembejeo zao ikiwamo mbegu na kuthibiti matumizi ya mbegu feki, kuwezesha wakulima kupata pembejeo kwa wakati, kupata taarifa za afisa ugani katika maeneo yao pamoja na kuwasaidia wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao.

Wito huo umetolewa jana tarehe 7 Agosti 2023 na baadhi ya wakulima walioshiriki mafunzo ya namna ya kutumia mifumo hiyo katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Wakulima hao Innocent Michael kutoka Kasulu Kigoma na Justin Kitarima kutoka Kilolo Iringa wamesema mbali na faida za kuhakiki mbegu wanazotumia katika shamba yao kuwa ni halisi au feki, pia wamekuwa wakipata maelezo ya uhakika kuhusu mbegu hizo pamoja na huduma muhimu kutoka kwa maofisa ugani waliopo karibu yao.

“Ni kwa kutumia simu yako tu ya mkononi, haijalishi ni simu janja (smart phone) au simu ya kitochi, zote ukiingiza namba *148*52# unahakiki mfuko wa mbegu ulioununua pamoja na maelezo ya kutosha ambayo kwa hakika yametusaidia sana katika shughuli zetu za kilimo,”  amesema Michael ambaye ni mkulima wa mahindi na kiongozi wa kikundi cha wakulima wapatao 100 kutoka Kasulu mkoani Kigoma.

Alisema baada ya kupatiwa mafunzo na kampuni ya Quincewood kuhusu mfumo wa T-Hakiki namna ya kuhakiki mbegu sasa wanalima huku wakiwa na uhakika wa kupata mavuno bora kutokana na kutumia mbegu bora zilizohakikiwa pamoja na maelekezo sahihi kutoka kwa watalaamu wa ugani kupitia mfumo huo wa Wakala Digital.

Alisema alipoanza kujiunga na mfumo huo, yeye pamoja na wenzie walifundishwa namna ya kujisajili na kupata huduma za mabwana shamba (maofisa ugani) sambamba na uhakiki wa mbegu kabla ya kuzitumia.

“Tunapata maelezo ya kutosha kuanzia tarehe ya kutengenezwa kwa mbegu hizo na muda wa kuisha kwake, kiujumla tunapata maelezo ya kutosha na mkulima kuamua kufanya uchaguzi wake. Hakika T- HAKIKI  na hawa Wakala Digital wametusaidia sana,” alisema.

Maelezo hayo ya Michael yanaungwa mkono na mkulima wa mahindi, nyanya na mazao mengine, Justin Kitarima ambaye alisema ni dhahiri Wakala digital wamewapatia kitu ambacho wanakwenda kukitumia kuwaelimisha wenzao.

“Pia naishukuru (TOSCI) Taasisi ya udhibiti ubora wa mbegu Tanzania kwa kuwa nasi bega kwa bega na kutupatia elimu kuhusu matumizi ya mbegu mbalimbali na hata kutufundisha pia namna ya kutumia mifumo hii ya kiteknolojia (T-Hakiki) hali ambayo inatuwezesha kukuza kilimo chetu kibiashara,” alisema.

Aidha, akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Quincewood Group Limited, Fatma Fernandes alisema wamekuwa na muendelezo wa kutoa mafunzo hayo ya namna ya kutumia mifumo ya kidijitali T-HAKIKI na mfumo wa Wakala Dijital ili kuwawezesha wakulima kupiga hatua na kulima kibiashara. 

Alisema mafunzo hayo yana faida kubwa kwa sababu wanawafundisha wakulima kuwa pindi wanaponunua mbegu ni muhimu wahakiki uhalisi wa mbegu hizo kabla ya kuzitumia.

“Sisi Quincewood tunafanya kazi na TOSCI, tunatoa elimu kwa wakulima ili waweze kuhakiki mbegu wanayopendelea kulima. Hii italeta tija katika sekta ya kilimo kwa sababu tunatokomeza matumizi ya mbegu feki kwenye sekta hii. Kupitia ubunifu huu wa T-Hakiki, mbegu feki imepungua sana nchini” alisema.

Aidha, Fatma ambaye ameshiriki maonesho hayo ya wakulima nanenane zaidi ya mara sita, alisema awali walipoanza kuutambulisha mifumo ya kidigitali na masuala ya kiteknolojia watanzania wengi walikuwa hawaelewi.

“Lakini kwa kweli sasa nampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukigeuza kilimo kuwa biashara, pia nampongeze Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwa kuhakikisha wanawake na vijana tunaingia kwenye kilimo na kutambua mifumo hii ya kiteknolojia kuboresha sekta hii. Tunaona kabisa kuwa kilimo kinalipa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here