Home LOCAL SERIKALI, BUNGE WAAZIMIA KUTOKOMEZA MALARIA IFIKAPO 2030

SERIKALI, BUNGE WAAZIMIA KUTOKOMEZA MALARIA IFIKAPO 2030

Na: WAF, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na kamati ya afya ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejadili afua za kutokomeza Malaria ifikapo Mwaka 2030 ili kuendelea kuimarisha sekta ya afya nchini.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 19, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo wakati akifungua kikao cha siku Mbili chenye lengo la kujenga uwezo Kwa Wabunge na wajumbe wa Baraza la kutokomeza Malaria.

Aidha Mhe. Nyongo amesema kamati ya bunge itashirikiana na Serikali katika kutokomeza malaria kwa kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kutumia dawa za viua wadudu ili kuondoa mabaki na mazalia ya mbu.

“Serikali, Bunge na wadau wanapaswa kuweka nguvu na nia katika kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030 ili kuboresha zaidi Afya za Watanzania na hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa letu” amesema Mhe. Nyongo

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel amesema amesisitiza katika kutumika vyema kwa rasilimali ambazo serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani jitihada za kutafuta pesa ni kubwa katika kuboresha sekta ya afya nchini.

Aidha, Dkt. Mollel amelitaka Baraza la kutokomeza Malaria nchini kusimamia vizuri rasilimali zilizopo za kutokomeza Malaria ili kufikia malengo ya kuutokemeza ugonjwa huo ifikapo 2030.

“Serikali chini ya Rais Dkt. Samia inahangaika kutafuta hela na kununua rasilimali ili kusaidia kutokomeza Malaria sasa ni vizuri mkazisimamia rasilimali zilizopo” ameongeza Dkt. Mollel.

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Kutokomeza Malaria nchini Eng. Leodegar Tenga amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo kutokana na malaria licha ya changamoto zilizopo, hii ni kufuatia jitihada za Serikali na Wadau katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria nchini.

“Sisi Kama Baraza tunatambua kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo kutokana na malaria, licha ya changamoto zilizopo ikiwemo za kupata rasilimali”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here