Home BUSINESS MIGODI MIKUBWA YENYE UBIA NA SERIKALI YACHANGIA SHILINGI TRILIONI 1.53 KUFIKIA JUNI,...

MIGODI MIKUBWA YENYE UBIA NA SERIKALI YACHANGIA SHILINGI TRILIONI 1.53 KUFIKIA JUNI, 2023

Katibu Mkuu Mahimbali aeleza Mipango Kabambe kuendeleza Sekta ya Madini, aeleza Miradi Mingine Mbioni kupewa Leseni

Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa hadi kufikia Juni, 2023 miradi ya uchimbaji mkubwa wa madini ambayo Serikali ina hisa imechangia mapato ya Serikali ya jumla ya Shilingi Trilioni 1.53 ambayo yametokana na tozo na kodi mbalimbali.

Mahimbali ameyasema hayo Agosti 21, 2023 jijini Dodoma kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya uendeshaji wa migodi ambayo Serikali ina hisa na mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inahuisha mikataba katika migodi mikubwa ili iendane na mabadiliko yaliyofanyika kwenye Sheria ya Madini pamoja na Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili, 2017.

 

Ameongeza kwamba, mbali ya kuchangia kodi, migodi hiyo imewezesha kutoa ajira zipatazo 3,110 kwa watanzania na kuchangia kiasi cha shilingi 21, 045, 546,929.42 ikiwa ni mchango kutokana na Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) pamoja na kutumia jumla ya shilingi 2, 893,423, 283, 326.05 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa na huduma nchini.

Ameitaja migodi hiyo kuwa ni North Mara, Buzwagi, na Bulyanhulu inayochimba madini ya dhahabu kupitia Kampuni ya Twiga Minerals Corporation Limited , kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya nikeli katika eneo la Kabanga wilayani Ngala, Faru Graphite Corporation Limited itakayojihusisha na uchimbaji wa madini ya Kinywe wilayani Mahenge na Mamba Minerals inayojihusisha na uchimbaji wa madini adimu yaani ( Rare Earth Elements ) katika eneo la Nguala mkoa wa Songwe.

‘’Mhe. Mwenyekiti migodi mingine yenye hisa na Serikali iliyochangia mapato hayo ni kampuni ya Sotta Mining Limited kupitia mgodi wa Nyanzaga uliopo Wilayani Sengerema, na kampuni ya Williamson Diamond Limited (WDL) kupitia mgodi wa Mwadui uliopo Mkoa wa Shinyanga.

Aidha, Mahimbali ameieleza kamati hiyo kwamba, katika kuhakikisha Serikali inanufaika na uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini na kusimamia utekelezaji kulingana na matakwa ya Sheria ya Madini, Serikali inatarajia kutoa leseni za uchimbaji wa madini kwa kampuni za Duma TanzGraphite na Nyati Minerals Sand Limited zitakazofanya uchimbaji mkubwa pamoja na Kudu Graphite Limited itakayofanya uchimbaji wa Kati na kuongeza kwamba, Serikali itakuwa na umiliki wa hisa za asilimia 16 kwa kila mradi.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mahimbali ameieleza Kamati hiyo mikakati ya Wizara kuiendeleza Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inaifungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyinigne za kiuchumi na kuzitaja baadhi kuwa ni Kilimo ambapo rasilimali madini hutumika katika uzalishaji wa mbolea kwa matumizi ya kilimo. Aidha, ametumia fursa hiyo kuishukuru kamati hiyo kutokana na ushauri na maelekezo yake ambayo yameiwezesha Sekta ya Madini kuendelea kufanya vizuri ikiwemo kupata tuzo tatu zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Agosti Agosti, 2023 kwa taasisi zilizofanya vizuri ambapo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya Twiga zilipata ushindi wa kwanza kupitia vipengele mbalimbali .

Akijibu hoja iliyotolewa na Kamati kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dunstan Kitandula na wajumbe wengine la kuiwezesha STAMICO kusimama kwa niaba ya Serikali katika kampuni za uchimbaji mkubwa na wa kati wa madini badala ya kuanzisha kampuni nyingine tanzu, amesema kuwa Serikali imeyachukua maelekezo hayo na pia wizara ina mpango wa kuiwezesha STAMICO kuwa na ushindani na kampuni kubwa za nje ikiwemo kuiwezesha kuvuka mipaka ya ndani na kuwekeza katika mataifa mbalimbali barani Afrika.

‘’Mhe. Mwenyekiti suala hili litafuatiliwa kwa umakini na kwa kuzingatia taratibu, maelekezo haya ni dhabiti na yataongeza tija kwenye Sekta ya Madini.’’amesema Mahimbali.

Kuhusu suala la kuhakikisha miradi ya madini inatekelezwa hususan ile inayotarajia kuanza utekelezaji, amesema Wizara imeweka mazingira ambayo yatawasaidia wawekezaji kuweza kufanya shughulli zao kikamilifu kulingana na muda uliopangwa.

Akizungumza katika kamati hiyo, Mwenyekiti Kitandula ameitaka Wizara kuendelea kuwajengea wajumbe wa kamati hiyo uelewa kuhusu shughuli na miradi inayotekelezwa na wizara na wadau ili kupata uelewa wa pamoja na kuiwezesha kamati hiyo kusimamia na kuishauri Sekta ya Madini kikamilifu.

Previous articleRAIS WA INDONESIA AWASILI NCHINI TAYARI KWA ZIARA YA KITAIFA YA SIKU MBILI
Next articleTANZANIA KUWA KITOVU CHA UCHAKATAJI MADINI BARANI AFRIKA – DKT. KIRUSWA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here