Home BUSINESS MAUZO YA MKONGE NJE YA NCHI YAPAA, WAINGIZA DOLA MILIONI 56.8

MAUZO YA MKONGE NJE YA NCHI YAPAA, WAINGIZA DOLA MILIONI 56.8

Afisa Kilimo wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Emmanuel Lutego akizungumza kuhusu mauzo ya mkonge nje ya nchi katika Maonesho ya Nanenane jijini Mbeya, katika Viwanja vya John Mwakangale ambako TSB inashiriki Maonesho hayo.

Na: Esther Mbusi, MBEYA.

Mauzo ya Mkonge nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 28,430.40 ambazo ziliingiza Dola za Marekani milioni 47. 7 mwaka 2021 hadi tani 32,627.35 mwaka 2022 ambazo ziliingiza Dola za Marekani milion 56.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.76 huku wakulima wadogo wakiongezeka.

Hayo yamebainishwa na Afisa Kilimo wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Emmanuel Lutego katika Maonesho ya Nanenane jijini Mbeya, katika Viwanja vya John Mwakangale ambako TSB inashiriki Maonesho hayo.

Amesema kwa sasa sekta ya Mkonge inazidi kukua ambapo hadi kufikia Juni mwaka huukumekuwa na ongezeko la wakulima wadogo wa Mkonge ambao wamefikia 11,979.

“Serikali imekuwa ikifanya hamasa kwa wakulima wapya katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Mara, Singida, Dodoma na mikoa mingine inayofaa kwa kilimo cha Mkonge ambapo imekuwa ikigawa mbegu bure kwa wakulima wa Mkonge ili kuongeza hamasa.

“Lakini pia serikali inafanya jitihada kubwa kurahisisha miundombinu ya usindikaji wa korona (mashine ya kuchakata Mkonge) ili kuongeza thamani kwa wakulima wapya na maeneo ambayo hayana miundombinu ya usindikaji wa mashine hiyo,” amesema.

Lutego amesema Serikali inaendelea kutoa msukumo mkubwa zaidi katika mitambo ya usindikaji ili kuongeza uzalishaji na kuongeza nyuzi zenye ubora zaidi ambazo zitasafirishwa katika masoko ya nje na ndani ya nchi.

Ili kurahisisha miundombinu ya uchakataji Mkonge kwa wakulima wadogo, amesema serikali imetenga katika bajeti zake fedha za kununua korona kubwa ambapo kwa kuanzia itaweka korona hiyo wilayani Handeni mkoani Tanga ambayo itatumika kuchakata mikonge yote ya wakulima wapya wanaowekeza katika wilaya hiyo na baadaye itawekeza katika wilaya za Mkinga na kisha kwenye mikoa mingine ya Singida, Dodoma na sehemu nyingine.

“Serikali katika bajeti yake imetenga zaidi ya Sh milioni 200 ili kukarabati korona ya Shamba la Kibaranga wilayani Muheza mkoani Tanga ili wakulima wadogo waweze kuchakata Mkonge kwa urahisi zaidi kwa hiyo serikali imekuwa ikifanya juhudi za kurekebisha na kufufua mitambo ili kuongeza uzalishaji Mkonge nchini,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here