Home Uncategorized MAKAMU WA RAIS AFUNGUA NANENANE 2023 MBEYA

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA NANENANE 2023 MBEYA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akiwasili katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya kufungua Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane nane leo tarehe 01 Agosti 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifungua Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane nane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya. (kutoka kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya Dkt. Stephen Mwakajumilo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera, Mke wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Spik awa Bunge Dkt. Tulia Ackson na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi David Silinde).

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akitembelea mambanda mbalimbali ya maonesho mara baada ya kufungua Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane nane leo tarehe 01 Agosti 2023 yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati alipotembelea banda la kilimo mara baada ya kufungua Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane nane leo tarehe 01 Agosti 2023 yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Asas Bw. Ahmed Asas alipotembelea banda la kampuni hiyo inayojishughulishaji na ufugaji wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane nane leo tarehe 01 Agosti 2023 yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wagunduzi wa mbegu bora zenye mchango mkubwa kwenye usalama wa chakula nchini waliopewa tuzo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane nane leo tarehe 01 Agosti 2023 yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia viongozi, wadau wa sekta ya kilimo na ufugaji pamoja na wananchi mbalimbali wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane nane leo tarehe 01 Agosti 2023 yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

MBEYA

Ndugu Wananchi, Kwanza, napenda kuwaletea salamu za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anawapongeza na kuwashukuru wakulima, wafugaji na wavuvi nchini kote kwa kazi nzuri ambayo inalihakikishia Taifa usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwanda, ajira, kipato na kuliingizia Taifa fedha za kigeni na kukuza uchumi wa nchi yetu.

Pili, napenda kuwashukuru Waheshimiwa na taasisi zifuatazo kwa maandalizi ya kiwango ya Nanenane 2023: Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo; Abdallah Hamis Ulega (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi; Juma Homera, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya; Wakuu wa Mikoa ya Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma, Rukwa na Katavi; viongozi na watumishi wa Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Maji, Viwanda na Biashara, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Kamati ya Maandalizi na Wananchi wote mliojitokeza kushiriki Maonesho haya.

Ndugu Wananchi;Kaulimbio ya Maadhimisho haya kwa mwaka 2023 inasema “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula”. Kaulimbiu hii inalenga kutukumbusha kuthamini mchango mkubwa wa Vijana na Wanawake katika shughuli za maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Kiuhalisia, vijana na wanawake ndiyo wanaochangia sehemu kubwa ya nguvu kazi katika uzalishaji, uchakataji, usambazaji na uuzaji wa chakula katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Wanawake Oyeee!! Vijana Oyeee!! Ndugu Wananchi; Katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020, Serikali imedhamiria kuendeleza Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na kukuza kipato na kutoa ajira kwa wananchi.

Kwa sababu hiyo, Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Shilingi 275 bilioni mwaka 2021/2022 hadi Shilingi 295 bilioni mwaka 2023/24 na ile ya Wizara ya Kilimo kutoka Shilingi 294,162,071,000 kwa mwaka 2021/2022 hadi Shilingi 970,785,619,000 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 330.02.

Mama Samia Oyeee!! Mifugo Oyeeee!! Kilimo Oyeeee!! Ongezeko hili linalenga kuimarisha maeneo mahsusi ya utafiti na huduma za ugani; kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi; kuimarisha na kutoa huduma ya upimaji wa afya ya udongo; kuendeleza kilimo cha umwagiliaji; kuimarisha upatikanaji wa Mitaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo; kuimarisha miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya kilimo; kuhamasisha na kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja na kuimarisha maendeleo ya ushirika.

Ndugu Wananchi, Mauzo ya mazao ya chakula yamekuwa chanzo cha ongezeko la fedha za kigeni katika uchumi wa nchi yetu. Mathalan, thamani ya mauzo ya mahindi nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani 57,097,279 kwa mwaka 2021 hadi Dola 71,543,641 mwaka 2022 na thamani ya mauzo ya ufuta kutoka Dola za Marekani 123,000,627 mwaka 2021 hadi Dola 143,788,838 mwaka 2022.

Hivyo, natoa rai kwa wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili nchi yetu iweze kujitosheleza kwa chakula na kupata fedha zaidi za kigeni kutokana na mazao mbalimbali. Ndugu Wananchi, Katika kuongeza matumizi ya mbolea nchini, Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji na kuhimiza matumizi ya mbolea kupitia Mpango wa ruzuku ili kuongeza tija na uzalishaji.

Kupitia Mpango huo matumizi ya mbolea kwa mwaka 2022/2023 yamefikia tani 580,628 ikilinganishwa na tani 363,599 kwa mwaka 2021/2022. Aidha, katika mwaka 2023/2024 Serikali itaendelea kuwezesha upatikanaji wa mbolea nchini kupitia Mpango wa ruzuku.

Ndugu Wananchi; Kwa kutambua mchango wa vijana na umuhimu wa kuongeza fursa za ajira, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeanzisha mradi wa Jenga Kesho Iliyo bora (Building a Better Tomorrow – BBT).

Katika mradi huu (kwa upande wa Wizara ya Kilimo) kuna vituo Atamizi 13 ambapo vijana 812 (wanawake 282 na wanaume 530) wameanza mafunzo ya kilimo biashara. Aidha, kwa upande wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi jumla ya vituo atamizi nane (8) vyenye jumla ya vijana 238 (71 Wanawake na 167 Wanaume) wanaendelea na mafunzo ya unenepeshaji wa mifugo.

Lengo la vituo hivi ni kuwawezesha vijana kupata uzoefu katika kuanzisha na kuendesha miradi ya kilimo na ufugaji kibiashara pamoja na kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mazao bora ya mifugo, malighafi kwa ajili ya viwanda nchini na kuongeza fursa za kujiajiri.

Ndugu Wananchi; Serikali yetu inaendelea kutoa programu ya mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa vijana kwa kushirikiana na Sekta binafsi ambapo jumla ya vijana 200 (74 wanawake na 126 wanaume) wamepatiwa mafunzo haya na mpango wa Serikali ni kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana 750.

Aidha, kwa dhati kabisa namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kwa uamuzi wake wa kutoa msukumo katika uwezeshaji wa vijana kupata ajira kupitia miradi ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow – BBT), kwa upande wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Hivyo, nawasihi vijana kuchangamkia fursa hizi ili kujipatia ajira na kukuza uchumi wao binafsi na wa Taifa kwa ujumla.

Aidha, nazielekeza Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi kuona namna bora ya kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili vijana wa JKT wanaojitolea wapewe kipaumbele kushiriki katika programu hii.

Ndugu Wananchi;Eneo lingine muhimu ni huduma za ugani ambazo ni kiungo muhimu katika kuwezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kuongeza uzalishaji na tija.

Katika hotuba yangu ya ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane ya mwaka 2022 katika viwanja hivi, nilisisitiza kuhusu wajibu wa Maafisa Ugani kupeleka huduma zao kwa wakulima/wafugaji badala ya kusubiri kufuatwa.

Hata hivyo, licha ya changamoto kadhaa zinazoathiri utoaji wa huduma za ugani nchini, naendelea kusisitiza kuhusu kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima wetu.

Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za ugani kwa kuwapatia Maafisa Ugani vitendea kazi mbalimbali vikiwemo pikipiki, vifaa vya matibabu, uhimilishaji na vifaa vya kupima afya ya udongo.

Aidha, ninaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kuwapatia mafuta na kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya pikipiki hizo.

Ndugu Wananchi; Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji nchini ikiwemo kujenga mabwawa ya kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya umwagiliaji, ambapo lengo ni kufikia eneo la umwagiliaji la hekta 1,200,000 ifikapo mwaka 2025.

Hadi sasa, Serikali imefikia asilimia 60.6 sawa na hekta 727,280.6 za eneo linalomwagiliwa.

Wito wa Serikali kwa wananchi ni kutumia na kutunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kusaidia kuleta tija.

Ndugu Wananchi; Kwa kutambua umuhimu wa ushirika katika kuwaweka wakulima pamoja, Serikali inaendelea kuhamasisha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kujiunga na Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) vitakavyokuwa chanzo cha mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao na kuimarisha uwekezaji katika kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Aidha, ili kuimarisha upatikanaji wa mitaji, Serikali inaendelea kuhamasisha na kuzitaka taasisi za fedha kubuni bidhaa/huduma zitakazowawezesha wananchi wengi kukopa ili kukuza mitaji yao.

Natumia fursa hii kupongeza mabenki ambayo yameanza kutekeleza jukumu hili na nazisisitiza taasisi zote za fedha kuendelea kupunguza riba ili wakulima, wafugaji, wavuvi, wasindikaji, wanunuzi na wajenzi wa viwanda waweze kukopa.

Aidha, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iongeze kasi ya kutoa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo.

Ndugu Wananchi; Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa ambayo inaathiri shughuli za uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Hali hii inachangiwa na shughuli za binadamu ikiwa ni pamoja na kilimo kisichozingatia uhifadhi wa mazingira, ufugaji usiozingatia ukubwa wa eneo, ufugaji wa kuhamahama, uvuvi haramu, ufugaji wa viumbe maji katika maeneo yasiyoidhinishwa kisheria, ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Katika suala hili, nawahimiza wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi wote kuwa mstari wa mbele kutunza mazingira, kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti, kufuga mifugo kulingana na ukubwa wa eneo, kulima malisho ya mifugo yenu na kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia za kilimo, mifugo na uvuvi zinazohimili mabadiliko ya tabia nchi.

Ndugu Wananchi; Kabla ya kuhitimisha hotuba hii, ninapenda kuwafahamisha kuwa nchi yetu itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika kwa mwaka 2023 (African Food Systems Forum), utakaofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 8 Septemba, 2023 Jijini Dar es Salaam.

Hii ni heshima kwa nchi yetu na fursa ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Nawahimiza wadau wote wa sekta hizi hususan sekta binafsi kuchangamkia fursa ya kushiriki katika jukwaa hilo litakalokuwa na washiriki wasiopungua 3,000 kutoka nchi mbalimbali.

Ndugu Wananchi; Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kutoa msisitizo wa masuala muhimu yafuatayo: Jambo la Kwanza, makundi makubwa ya mifugo yameingizwa katika mikoa ya nyanda za juu kusini! Madhara yake ni makubwa sana, ikiwemo kuharibiwa sana kwa mazingira.

Aidha, imezuka migororo mingi kati ya wakulima na wafugaji. Migororo hii imepelekea uharibifu wa mazao, mifugo na binadamu kuuawa au kujeruhiwa.

Wanyama kama Tembo nao wanakimbia bugudha ya mifugo na sasa wanahamia kwenye makazi ya binadamu wakiharibu mazao na hata kuua watu. Hivyo, Wizara zote husika na Wakuu wa Mikoa wachukue hatua thabiti kudhibiti uingizaji mifugo kinyemela katika maeneo yao ya utawala.

Aidha, watenge na kupima vitalu/mashamba ya mifugo na kushirikiana na wamiliki wa mifugo kujenga malambo na kuendeleza malisho na pia kuuza mifugo ya ziada. Jambo la Pili, matumizi sahihi ya viuatilifu na kemikali. Kumekuwepo matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu na kemikali nyingine.

Jambo hili lina athari kubwa kwa afya ya binadamu na viumbe hai vingine. Nawasihi wakulima, wafugaji na wavuvi kuzingatia maelekezo ya wataalam ili tuweze kuzalisha pasipo kuathiri afya ya binadamu na mazingira yetu.

Jambo la Tatu, kuenea kwa mtindo wa kubadili matumizi ya ardhi iliyotengwa mahsusi kwa ajili ya Utafiti Kilimo.

Maeneo mengi ya taasisi za utafiti yamevamiwa na kupimwa viwanja! Jambo ambalo linatishia utafiti wa kilimo na mifugo kwa kuwa vituo vyetu vya utafiti vitakosa maeneo ya kutosha ya kufanyia kazi.

Ndugu zangu Watanzania lazima tutambue kuwa kilimo ni Sayansi na Utafiti Kilimo usipopewa kipaumbele basi mapinduzi ya kilimo yatabaki kuwa ndoto.

Hivyo, maeneo ya taasisi za Utafiti Kilimo yapimwe, yapewe hati miliki na yalindwe.

Vivyo hivyo, kuna uhaba wa maeneo mahsusi ya kuzalishia mbegu.

Hii inatokana na kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa kutenga maeneo kwa madhumuni ya uzalishaji wa mbegu na pia utunzaji wa yale yaliyopo.

Kwa kuwa maeneo ya uzalishaji wa mbegu si kama maeneo ya kilimo cha mazao ya kawaida, naelekeza Mamlaka zinazohusika pia kutenga na kupima ardhi kwa ajili ya madhumuni hayo na kuyalinda dhidi ya uvamizi.

Jambo la Nne, usalama wa chakula katika kaya. Nasisitiza wananchi kutouza chakula chote na badala yake kuhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi ya kaya. Kuhakikisha usalama wa chakula katika kaya uwe wajibu wa msingi wa kila kaya nchini.

Aidha, kwa mazao ya kibiashara nawasihi wakulima kutoyauza kabla ya kukomaa na kufikia ubora unaokubalika. Hii ni muhimu ili kutoharibu soko la mazao yetu ndani na nje ya nchi.

Naelekeza Wizara ya Kilimo kuweka utaratibu mzuri wa kuhakiki ubora wa mbegu zinazouzwa na mazao. Jambo la Tano, ni tatizo la uhaba wa mbegu za malisho na mbegu bora za mifugo vikiwemo vifaranga vya Samaki. Tatizo hili linakwamisha juhudi za kukuza na kupanua kilimo na ufugaji kwa kiasi kikubwa.

Naelekeza Wizara husika na taasisi za utafiti wa mifugo na viumbe maji kuhakikisha mbegu za malisho na mifugo zinapatikana kwa wananchi na kwa gharama nafuu.

Ndugu Wananchi, Nimefarijika na nimeridhika na kiwango cha maandalizi ya maonesho haya. Nawahimiza wananchi wa Jiji la Mbeya na Mkoa mzima waje kutembelea maonesho haya, wajifunze na kujionea bidhaa mbalimbali za kilimo na mifugo lakini pia fursa nyingi zilizoko katika sekta hizi kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa letu.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa Maonesho na sherehe za Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kwa mwaka 2023 yamefunguliwa rasmi. Asanteni kwa kunisikiliza

Previous articleWIKI YA AZAKI 2023 YAZINDULIWA RASMI JIJINI DAR 
Next articleMAKAMU WA RAIS KATIKA BANDA LA BoT MAONESHO YA NANENANE MBEYA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here