Home BUSINESS KIGAHE  AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUWA WAADILIFU KATIKA HUDUMIA ZAO 

KIGAHE  AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUWA WAADILIFU KATIKA HUDUMIA ZAO 

Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) Agosti 9, 2023 akipeana mkono na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Dkt. Fransis Michael kama ishara ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya viwanda na biashara wakati wa ziara yake ya siku mbili katika Mkoa huo Agosti 9 – 10, 2023.

Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) Agosti 9, 2023 akisikiliza maelezo ya Kaimu Meneja Msaidizi Mamlala ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Songwe Bw. Joseph Maleko kuhusu ushuru wa forodha katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (OSBP) pamoja na changamoto zilizopo katika kuimarisha biashara mpakani wakati wa ziara yake ya siku mbili katika Mkoa huo Agosti 9 – 10, 2023.

Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) (kulia)   akisikiliza maelezo ya Afisa Uhamiaji Mfawidhi Idara ya Uhamiaji Tunduma Mrakibu Deodatus Sonda ( kushoto) kuhusu huduma za uhamiaji zinazotolewa katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (OSBP) pamoja na changamoto zilizopo katika kuimarisha biashara mpakani wakati wa ziara yake ya siku mbili katika Mkoa huo Agosti 9 – 10, 2023.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe ameziagiza Taasisi za Umma kuendelea kutoa huduma kwa wafanyabiashara kwa weledi na uadilifu ili kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Vile vile amewaagiza Maafisa wa Taasisi zinazohudumia Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani Tunduma (OSBP) kupunguza vikwazo vya kibiashara visivyo vya lazima kwa wafanyabiashara wanaotumia kituo hicho kinachohudumia Nchi sita zikiwemo Zambia, Zimbabwe Congo-DRC, Botswana, Afrika Kusini na Namibia ili kukuza biashara za mpakani na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hizo na kuongeza mapato.

Kigahe ameyasema hayo Agosti 9, 2023 wakati wa ziara yake katika Mkoa wa Songwe ambapo alitembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Wakala wa Vipimo (WMA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (OSBP) Tunduma ili kujionea utendaji kazi, kusikiliza na kutatua changamoto zilizopo.

Aidha, amezielekeza Taasisi za WMA na SIDO kuhakikisha zinafungua Ofisi katika Mkoa wa Songwe ili kurahisisha utoaji wa huduma za taarifa, mafunzo, mikopo na matumizi sahihi ya vipimo kwa wajasiliamali wa Mkoa huo ili kukuza biashara zao na kuongeza pato la Taifa.

Awali akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Dkt Fransis, Kigahe amesema Wizara yake pamoja na Taasisi zake itaendelea kushirikiana na uongozi wa Mkoa huo ili kuhakikisha kuwa Mkoa huo wa Kimkakati unakuwa na mazingira bora ya biashara na uwekezaji.

Aidha Mhe. Kigahe ameielekeza TBS kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini ziwe na ubora unaotakiwa kulingana na viwango vinavyokubalika kimataifa bila kuathiri Sheria Kanuni na Taratibu zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCFTA) na Jumuiya nyinginezo.

Vilevile ameiagiza WMA kukagua bidhaa zinazoingia nchini kulingana na vipimo vilivyoandikwa kwenye label ili kulinda afya za Watanzania na kuhakikisha bidhaa wanazonunua zinaendana na thamani ya pesa.

Kigahe pia amewashauri wakulima na wafanyabiashara wa Mkoa wa Songwe kuunda vikundi au vyama vya msingi ili waweze kupata mikopo ya mizani zitakazowawezesha kuuza bidhaa zao katika vipimo sahihi , kupata faida inayostahili na kuondokana na changamoto ya Lumbesa pamoja na kuchangia katika pato la Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here