Home BUSINESS BoT: TANZANIA INA AKIBA YA KUTOSHA YA FEDHA ZA KIGENI

BoT: TANZANIA INA AKIBA YA KUTOSHA YA FEDHA ZA KIGENI

Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango, akitoa wasilisho lake kuhusu masuala ya fedha za kigeni kwenye kikao na wahariri, waandishi wa habari na wadau wa sekta ya fedha nchini, makao makuu ndogo ya BoT Jijini Dar es Salaam Agosti 22, 2023. 

NA: K-VIS BLOG, DAR ES SALAAM

NCHI ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, ameeleza Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango.

“Pamoja na kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni nchini, hususan dola ya Marekani, hali ya upatikanaji wa fedha za kigeni umeendelea kuwa himilivu,” amesema Dkt. Missango katika kikao na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam le Agosti 22, 2023.

Amesema uhimilivu huo unatokana na kuendelea kuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni nchini, ambapo hadi Jumatatu tarehe 21 Agosti 2023, akiba hiyo ilikuwa dola za Marekani milioni 5,441.

Akiba hiyo, “inatosheleza miezi 4.9 ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje. Kiasi hiki kinalingana na kipindi kabla ya changamoto ya uchumi wa dunia zilizopelekea kuwepo kwa upungufu wa fedha za kigeni,” alibainisha.

Aidha, mkurugenzi huyo amesema Benki Kuu inaendelea kutumia akiba iliyopo kuongeza ukwasi katika soko la fedha za kigeni nchini.

“Kuanzia mwezi Julai hadi Agosti 21, 2023, Benki Kuu imeuza katika soko la fedha za kigeni dola milioni 100.5, ikilinganishwa na dola milioni 62 katika kipindi cha Julai-Septemba 2022,” ameeleza Dkt. Missango.

Amesema tangu kuanza kwa vita ya Ukraine mwezi Machi 2022, Benki Kuu imekwisha uza katika soko la fedha za kigeni dola milioni 518.5.

Katika kikao hicho ambacho pia kiliwashirikisha wawakilishi wa mabenki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni bara na visiwani, Dkt. Missango amesema Serikali na Benki Kuu zinaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni nchini.

“Hatua hizo ni pamoja na Benki Kuu kuongeza kiwango cha kuuza fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni, kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu na  mikakati ya kuongeza mauzo nchi za nje na kuzalisha bidhaa mbadala wa zile zinazoagizwa nje ya nchi,” ameeleza.

Ameeleza matumaini yake kwamba uchumi wa dunia umeanza kuimarika, na hivyo kuashiria kuanza kuwepo kwa ongezeko la fedha za kigeni nchini.

Amesema ukuaji wa uchumi wa dunia unatarajiwa kufikia asilimia 3 mwaka 2023 tofauti na matarajio ya awali ya ukuaji wa asilimia 2.8.

Aidha, bei za bidhaa katika soko la dunia zimeendelea kupungua, na mfumuko wa bei umeendelea kupungua katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Ameeleza pia kwamba, benki kuu za nchi mbalimbali duniani, ikiwemo Marekani, zimeanza kupunguza kasi ya kuongeza riba katika kukabiliana na mfumuko wa bei.

“Mwenendo huu wa kuridhisha katika uchumi wa dunia, unaashiria kupungua kwa changamoto ya upungufu wa dola ya Marekani nchini.

Pamoja na maendeleo hayo duniani, uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika na kuna viashiria vya kupungua kwa changamoto za upungufu wa fedha za kigeni nchini.

Benki Kuu ya Tanzania imewataka wananchi kuondoa hofu ya upatikanaji wa fedha za kigeni.

Aidha imeviomba vyombo vya habari kutoa taarifa sahihi ili kuepusha hofu na taharuki katika upatikanaji wa fedha za kigeni nchini.

Wafanyabiashara na wananchi wametakiwa kuzingatia sheria, miongozo na kanuni za fedha za kigeni kama zilivyoanishwa katika tamko kuhusu matumizi ya fedha za kigeni nchini na taarifa ya Benki Kuu kwa umma ya tarehe 20 Juni 2023 na kwamba fedha zitokanazo na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi kuwekwa katika mabenki hapa nchini.

Aidha, Benki Kuu imewataka wananchi kuongeza matumizi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini.

“Hatua hii itapunguza mahitaji ya fedha za kigeni, kuimarisha shughuli za uchumi, na kuongeza kipato kwa wananchi,” amesema Dkt. Missango na kuwataka wazalishaji kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa na huduma ili kupunguza uhitaji wa bidhaa au huduma kutoka nje na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Katika kikao hicho, wahariri walipata nafasi ya kuuliza maswali ambayo yalijibiwa kwa pamoja na Benki Kuu na wawakilishi wa mabenki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.

Upungufu wa fedha za kigeni nchini, kama ilivyo duniani kote umetokana na athari za vita kati ya Urusi na Ukraine, UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi, na mabadiliko ya mwelekeo wa sera ya fedha katika kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei duniani.

(CREDIT: K-VIS BLOG/KHALFAN SAID)

Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango (katikati kulia), akitoa wasilisho lake kuhusu masuala ya fedha za kigeni kwenye kikao na wahariri, waandishi wa habari na wadau wa sekta ya fedha nchini, makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam Agosti 22, 2023 Bw. Alex Ngw’inamila, Mkuurgenzi waMasoko ya Fedha BoT.

Bw. Alex Ngw’inamila, Mkuurgenzi waMasoko ya Fedha BoT.

Bw. Sadat Musa, Mkurugenzi wa Usimamizi Sekta ya Fedha BoT.

Bw. Lameck Kakulu, Meneja Masoko ya Fedha BoT.

Bi.Villela Vaane, Meneja anayeshughulikia Uchumi wa Kimataifa na Sekta za Uzalishaji, BoT.

Bw.Lekinyi Mollel (kushoto), Meneja wa Bajeti na Madeni, BoT, akifafanua jambo.  

Baadhi ya wadau kutoka sekta ya fedha nchini

Bw. Suleiman Mohammed (wapili kushoto) kutoka duka la kubadilisha fedha za kigeni, Furaha Safari la Unguja, Zanzibar, akizungumza kwenye kikao hicho.

Bw. Deogratius Marandu (kushoto),  wa dula la kubadilisha fedha za kigeni la Kadoo, akichangia katika kikao hicho.

(PICHA ZOTE NA: KHALFAN SAID)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here