Na: Catherine Sungura, Dodoma
Shirika la Afya Duniani (WHO) kuipatia Tanzania fedha Za kitanzania milioni 855 kwa ajili ya kuwezesha kufanya utafiti wa kitaifa wa viashiria vya Magonjwa Yasiyoambukiza (Steps Survey 2023) unaotarajiwa kuanza mapema Agosti, mwaka huu nchi nzima
Akiongea wakati wa uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe.Nassor Mazrui jijini Dodoma,Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Prof. Said Abood amesema fedha hizo zitazaidia kukamilisha zoezi hilo kwa Tanzania Bara na Zanzibar .
Prof.Abood amesema kuwa Utafiti wa “Steps Survey” ni ufuatiliaji wa viashiria vya Magonjwa Yasiyoambukiza ili kukusanya takwimu muhimu kuhusu Magonjwa yasiyoambukiza na viashiria vya hatari vya magonjwa hayo.
“Tafiti hii itatoa taarifa muhimu kuhusu hali ya afya na jamii yetu na kutambua matendo ya maboresho katika afya na kuweka mikakati kwa ajili ya kuboresha Matendo hayo kwa lengo la kuimarisha afya ya Jamii yetu,” alisema Prof. Abood
Alisema takwimu ndio kiini cha kujenga Taifa lenye afya bora. “Takwimu tutakazokusanya kupitia Utafiti huu zitatumika kama dira ya kutuongoza kuelekea kutengeneza mikakati yenye ushahidi ili kuboresha afya za watanzania.
Vile vile alisema takwimu zitawafanya kuelewa viashiria vya hatari vya magonjwa yasiyoambukiza kama vile ulaji usiofaa, kutokufanya mazoezi ya mwili na unywaji wa pombe kupita kiasi na kunaweza kubuni mbinu zitakazoshughulikia visababishi hivyo vikuu vya NCDs.
Naye, Mwakilishi wa WHO Dkt. Alphoncina Nanai alisema Magonjwa Yasiyoambukiza yameanza kuwa tatizo kubwa ulimwenguni.
Alisema katika kila vifo 10, vifo 7 vinasababishwa na magonjwa Yasiyoambukiza ulimwenguni na watu milioni 17 wanafariki ambapo 86% ya vifo vinatoka nchi za Afrika.
Aidha, Dkt. Nanai alisema Magonjwa Yasiyoambukiza yanaweza kuzuilika ndipo WHO na Serikali ilianzisha utaratibu wa kupima miaka kumi iliyopita ili kujua uzito wa magonjwa hayo na yanakuaje.
Alisema wanafuatilia magonjwa hayo kwani wapo watu wengi hawajui kama wana magonjwa hayo, magonjwa hayo kwa Sasa yanaua watu wengi
Alisema WHO itaendelea kushirikiana na Serikali ili kujua namma gani wataweza kuzuia magonjwa hayo kwa yeyote ambaye hajapata basi asipate na aliyepata aweze kutumia vizuri dawa
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge Huduma Za afya na Masuala ya UKIMWI Mhe.Stanislaus Nyongo alisema Utafiti huo utaenda kutatua changamoto la tatizo la magonjwa hayo na kuipa nchi dira.
Alisema kama Bunge wapo tayari kuelimisha wananchi kuepukana na magonjwa hayo ambayo hivi Sasa yanatumia pesa nyingi kuyatibu.