Home LOCAL WATAKWIMU NA WALIMU SKULI ZA MSINGI WATAKIWA KUJIFUNZA KWA BIDII

WATAKWIMU NA WALIMU SKULI ZA MSINGI WATAKIWA KUJIFUNZA KWA BIDII

MKURUGENZI Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Zanzibar,Bi.Mashavu Ahmada Fakih,akizungumza wakati akifungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu na Watakwimu wa Skuli za Msingi Wilaya za Mjini,Kati na Kusini Unguja(hawapo pichani) juu ya matumizi ya Mfumo wa kisasa wa maudhurio(Zanzibar Digital Attendance) yaliyofanyika katika kituo cha ubunifu wa Kisayansi kilichopo Jang’ombe (Picha na Is-haka Omar).          

NA: IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MKURUGENZI Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Zanzibar,Bi.Mashavu Ahmada Fakih,amewasihi watakwimu wa skuli za msingi na walimu nchini   kujifunza  kwa bidii mafunzo maalum ya mfumo wa kisasa wa kudhibiti na kufuatilia maudhurio ya wanafunzi waliorejeshwa skuli kuendelea na masomo ili kujua maendeleo na changamoto zinazowakabili.

Hayo ameyasema wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo watendaji hao yanayofanyika katika Kituo cha ubunifu wa kisayansi kilichopo skuli ya sekondari Jang’ombe, Wilaya ya Mjini Unguja.

 Bi,Mashavu, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa watendaji hao kwani yatawasaidia katika kufuatilia kwa kina muenendo wa maendeleo ya maudhurio kimasomo ya wanafunzi hao.

 Alieleza kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha watoto wote walioacha skuli kwa sababu mbalimbali wanapata haki ya elimu sambamba na kumaliza wimbi la watoto wa mitaani wasiojua kusoma na kuandika.

Katika maelezo yake Mkurugenzo huyo Bi.Mashavu, aliwasisitiza watendaji hao ambao ndio walimu wenye dhama za kujengea mazingira bora na rafiki wanafunzi hao kitaaluma,kimalezi na kiubunifu kuhakikisha wanajifunza kwa bidii kuelewa vizuri matumizi ya mfumo huo wa kiteknolojia unaoleta ufanisi mzuri wa kiutendaji.

“Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais wetu Dk.Hussein Ali Mwinyi, ameendelea kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo ndani ya sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha nchini inakuwa na mfumo bora na imara wa kielimu.

Walimu wenzangu tujitume na kujiongeza zaidi kwa kila hatua ya mafunzo yanayotolewa ili nasi twende sambamba na mabadiliko na matakwa ya Sayansi na Tekolojia kupitia kufundisha,kujifunza na kuongeza maarifa na ubunifu katika sehemu zetu za kazi”,alisema Mkurugenzi huyo na kuhimiza nidhamu,bidii na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Pamoja na hayo alisema kupitia mradi wa kuwarudisha watoto waliacha masomo skuli ni zaidi ya wanafunzi  30,000 wamerudi skuli na wanaendelea na masomo kwa ngazi mbalimbali za msingi na sekondari.

Kupitia mafunzo hayo Bi.Mashavu, alitoa wito kwa walimu,walezi na wazazi na kuwataka kuendeleza utamaduni wa kuwa karibu na wanafunzi wao ili kuwajenga wapende kusoma kwa bidii  kwa maslahi ya maisha yao.

Naye Mratibu wa Mafunzo hayo ya mfumo wa kisasa wa Maudhurio ya Wanafunzi Zanzibar Mohamed Ali Muombwa, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kitaaluma walimu hao wapate  kufuatilia,kuthibiti na kujua maudhurio ya wanafunzi hao kupitia njia ya kiteknolojia kupitia vifaa vya Vishikwambi na Komputer. Jumla ya walimu na watakwimu wa skuli za msingi 437 watapewa mafunzo hayo kwa awamu Unguja na Pemba.

                      MWISHO 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here