Ikunda Dionis Mushi, wa Shule ya Tiba na Kinywa, akitoa maelezo kwa washiriki wa maonesho, walipotembelea Banda ya UDOM.
Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakiwahudumia wananchi waliofika kwa wingi kwenye Banda lao, kupata maelezo ya programu na taratibu za udahili kwa mwaka wa masomo 2023/2024.
UDOM wakiwa katika utoaji huduma za afya kwa wananchi wanaotembelea maonyesho ya Vyuo Vikuu yanayoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Chuo Kikuu cha Dodoma, kinashiriki maonesho ya 18 ya Vyuo Vikuu nchini, yanayoratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania TCU.
Akizungumzia maonyesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bi. Rose Joseph, amesema wataalamu wa kila fani wanashiriki ili kutoa maelezo ya kina kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo kwenye Banda la Chuo hicho.
Amezitaja baadhi ya huduma muhimu zinazotolewa kwenye banda hilo kuwa ni udahili wa moja kwa moja wa wanafunzi wanaotaka kujiunga na Chuo hicho kwa Programu mbalimbali za masomo kwa mwaka 2023/24, ushauri wa kitaalamu kuhusu programu, huduma za malazi, na masuala mengine yanayohusu shughuli za Chuo Kikuu cha Dodoma.
Kwa sasa Chuo Kikuu Dodoma kinatoa mafunzo katika fani za Udaktari, Uchumi, Sheria, Sosholojia, Utawala wa Biashara, Biashara na Uhasibu, Biashara katika Utawala na Rasilimali Watu, ujasiriamali, Biashara ya Kimataifa, Utalii, Masoko, Mazingira, Takwimu, Ununuzi na Ugavi, Mawasiliano na Teknolojia (TEHAMA), Jiolojia, Kemia, Madini, Petroli, Nishati Mbadala, Elimu, lugha, Uhusiano wa Kimataifa, ikolojia, Uandishi wa Habari na Mahusiano ya Umma, fizikia, na nyinginezo.
Zaidi ya Programu 80 katika ngazi ya Shahada za Awali zinatolewa na UDOM, na kwa ngazi ya Shahada za Umahili (Postgraduate Diploma, Masters & PhD) Programu zaidi ya 56.
Bi, Rose amewakaribisha wananchi wa Dar es Salaam, Pwani na Mikoa Jirani kutembeela maonesho hayo kujifunza na kujiunga na programu mbalimbali za Chuo hicho, na kwamba huduma za ushauri ni Bure