Home BUSINESS TIC YAZIDI KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NCHINI, YAKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA ULAYA

TIC YAZIDI KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NCHINI, YAKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA ULAYA

Na: Beatrice Sanga, MAELEZO

Serikali imeendelea kujadiliana na wadau mbalimbali wa uwekezaji na biashara ili kuhakikisha kwamba wanaendelea na shughuli zao kwa ufanisi na bila bughudha.

Hayo yameelezwa July 18, 2023 Jijini Dar es Salaam na John Mathew Mnali Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji, uwekezaji Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) wakati wa mkutano uliowakutanisha kituo hicho, Ubalozi wa Uholanzi na Chama cha wafanyabiashara kutoka Ulayana wawekezaji, ambao ulikuwa na malengo ya kuwakutanisha wawekezaji kutoka Ulaya na Kituo cha Uwekezaji ili kupata ufahamu wa mambo mablimbali ya uwekezaji na taratibu mbalimbali za kuchukua ili kuweka mazingira mazuri kwaajili ya uwekezaji.

Mnali amesema kuwa malengo ya mkutano huo ni kuwakutanisha wawekezaji kutoka Ulaya pamoja na watoa huduma mbalimbali wa serikali wanaofanya kazi chini ya chini ya huduma za mahali pamoja, (One Stop Investment facilitation Center).

“Kama mnavyofahamu, pale kuna Taasisi kumi na moja ambazo zinawahudumia wawekezaji wanapokuja ili kuweza kupata leseni na vibali mbalimbali, sasa wawekezaji hawa huwa wanapata huduma hizo wanapokuja kwa mara ya kwanza lakini pia wanapoendelea kuishi hapa kwasababu kuna baadhi ya vibali vingine kama vibali vya kazi vinahitajika kuvihuisha kila baada ya muda fulani lengo hili kubwa ni kuweza kuwapa fursa sasa hawa wawekezaji wa nje ambao wako hapa kuweza kuzifahamu huduma zenyewe na pale wanapokutana na changamoto basi wajue ni afisa gani aliyepo TIC anashughulika na aina ya leseni anayoihitaji.”

Amesema kuwa wataendelea na utaratibu wa mikutano kama hiyo kwani imekuwa ikileta ufanisi katika shughuli za uwekezaji na ufanyaji biashara nchini, lakini pia imekuwa ikisaidia kufafanua mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakileta changamoto kwa wawekezaji.

Kwa upande wake Balozi wa Uholanzi nchini Wiebe de Boer amesema kuwa mijadala ya aina hiyo itazidi kuinua na kuleta uwekezaji wawekezaji nchini kwani watakuwa wana uelewa mkubwa juu ya mambo ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini Tanzania.

“Unaweza ukaona uwekezaji wa kigeni hapa Tanzania unazidi kupaa kila mwezi umekuwa na rekodi mpya ya ukuaji, na tunaamini hii hali itaendelea kuimarika, leo kulikuwa na Taasisi kumi na mbili ambazo wawekezaji wanapaswa kufanya nazo kazi, hivyo ni jambo jema sana maana linatupa taarifa mbalimbali, hivyo tunaamini kwamba TIC na Taasisi zake ziko katika njia nzuri ya kurahisisha zaidi mazingira ya uwekezaji Tanzania.”Amefafanua Balozi de Boer.

Naye Emma Oriyo Mkurugenzi Mtendaji wa European Business Group ambao ni wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya nchini, na ambao wamewekeza katika sekta mbalimbali kama kilimo, biashara na viwanda amesema kuwa wamefurahishwa na mkutano kwani umewapa nafasi ya kuelewa vitu mbalimbali na namna gani ya kukabiliana nazo.

“Lengo la kufanya mkutano huu leo ni kuleta karibu wawekezaji na wafanyabiashara kutoka bara la Ulaya ili waelewe kuhusu kazi ya one stop investment facilitation center lakini pia wapate msaada kutoka kituo hicho,”

Kituo cha Uwekezaji kimeeeleza kuwa kitaendelea kukutana na wawekezaji waliopo nchini na ambao wanatarajia kuja kuwekeza kuwekeza nchini ili kuhakikisha kuwa uwekezaji wao unaleta faida siyo kwao pekee bali kwa taifa pia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here