MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni, Shaweji Mkumbura . ameitaka jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Kinondoni, kuanza mapema maandalizi ya chaguzi mbalimbali ikiwemo wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu kwa lengo la kupata ushindi wa kishindo.
Pia, alimshukuru Rais Dk. Samia kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya hiyo jambo ambalo limesababisha kuleta mabadiliko makubwa.
Mwenyekiti Mkumbura aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana na wakati akifungua mkutano wa Baraza la Umoja huo Wilayanjni humo uliohusisha wajumbe na viongozi mbalimbali.
“Hakuna muda mrefu wakujipanga kuingia katika chaguzi mbalimbali, hivyo katika mambo yenu ikiwemo vikao, ajenda moja wapo iwe maandalizi ya Uchaguzi.
“Watu wengi wanaiangalia na kuipigia mahesabu Wilaya yetu, hivyo wasipo fanya jiandaa mapema tunaweza tusifanye vizuri, kwahiyo wakati ndio sasa wakujiandaa, “ alisisitiza
Aliwataka kufanya jitihada za kuongeza idadi ya wanachama kutokana na idadi kubwa ya watu walioko katika Wilaya hiyo, hivyo waweke mkakati mkubwa wa kuongeza wanachama.
“Tujipange tuache kukaa tu nyumbani, maofisini, bali tuzunguke kutafuta wanachama. Hakuna sababu ya kukaa maofisini, tufanye ziara za mara kwa mara kwenda kuwahamasisha wananchi,” alisema
Pia, alisisitiza uanzishaji wa miradi ya jumuiya kwani ni mikubwa, kuondoa hali ya utegemezi hivyo Wilaya hiyo inatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa wengine.
Aliwataka kuwa na nidhamu na kuheshimiana kwani hata Chama kimejengwa chini ya misingi ya nidhamu zaidi, hivyo kila mmoja anatakiwa kutekeleza hilo.
Aidha, amewataka kuendelea kutekeleza jukumu lao la kuongeza wanachama ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhai wa Jumuiya hiyo Wilayani humo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya hiyo, Anna Joseph alisema, wanaendelea kumuunga mkono Rais Dk.Samia katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk. Samia kazi yao kubwa ni kumpatia kura za kishindo mwaka 2025.
Kwa upande wake Katibu wa Umoja huo, Aziat Salim, alisema wanayomipango mbalimbali ya kkujiimarisha kiuchumi kwani hadi sasa wanavyo viwanja sita ambavyo wanakusudia kujenga miradi mbalimbali.