Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolfu Mkenda, (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, (kushoto) wakati alipokuwa akikagua Mabanda ya Taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizoshiriki Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, (katikati) akimsikiliza Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, (kushoto) alipokuwa akifafanua jambo wakati Waziri huyo alipofika katika Banda la TCU kufahamu mambo mbalimbali kuhusu maonesho hayo, aliyoyafungua rasmi Julai 18,2023 katika Viwanja vya mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, (kushoto) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika Banda la TCU katika Maonesho hayo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (kushoto), akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika viwanja vya mnazi mmoja kufungua rasmi maonesho ya Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia JUlai 18, 2023.
(PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO)
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda, ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuhakikisha kuwa Vyuo na Taasisi za elimu ya Juu nchini, vinaimarisha ushirikiano na Taasisi za utafiti na Sekta Binafsi, ili kuweka utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazoanzishwa nchini, na kuhamasisha matumizi yake ili kukuza na kuimarisha na kukuza kiuchumi katika jamii.
Profesa Mkenda ameyasema hayo Julai 18,2023 katika Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, yenye kaulimbiu isemayo, “Kukuza ujuzi nchini kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa uchumi imara na shindani”
Amesema kuwa wakati umefika kwa TCU kuhakikisha inasimamia tafiti na kutoa ushauri kwa vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu kote nchini. ili kuweza kutoa majibu ya changamoto zinazoikabili jamii kwa kuhamasisha matumizi ya Teknolojia itakayochochea maendeleo katika jamii.
Aidha amesema kuwa Serikali imeendelea kutenga fedha kwaajili ya mikopo ya Elimu ya Juu, na kuendelea kufanya maboresho makubwa ya elimu ili kuhakikisha kuwa kila mtanzania mwenye sifa anapata fursa ya kufikia malengo yake kielimu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Profesa Penina Mlamba amesema Serikali ipo kwenye mabadiliko ya mitaala na kwamba, TCU itaendelea kuchagiza Vyuo Vikuu kupokea mabadiliko hayo ili kuhakikisha vinaendelea kutoa elimu yenye ubora.
Maonesho hayo yameshirikisha Vyo na Taasisi za Elimu ya Juu zaidi ya 80 ambapo, yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi Julai 22, Mwaka huu.