Home BUSINESS SUA YATIA SAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO NA CHUO KIKUU CHA MWALIMU JULIUS...

SUA YATIA SAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO NA CHUO KIKUU CHA MWALIMU JULIUS NYERERE CHA KILIMO NA TEKNOLOJIA (MJNUAT)

NA: FARIDA MANGUBE, MOROGORO.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) wenye lengo la mashirikiano ya Kimitaala na Wahadhiri baina ya vyuo hivyo.
Zoezi hilo limefanyika Juni 9, 2023 katika Kampasi Mkuu ya Edward Moringe Sokoine mkoani Morogoro, likishuhudiwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini Mhe. Jumanne Sagini ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Butiama.
Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya Mitaala kati ya Chuo kikuu cha SUA na Chuo Kikuu cha MJNUAT Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema, makubaliano hayo baini ya SUA na MJNUAT ni utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu Kiongozi Moses Kusiluka la kuvitaka vyuo vyote nchini kushirikiana na kuacha kushindana.
Aidha Prof. Nombo amevitaka vyuo vingine nchini kuiga mfano wa Chuo Kikuu cha SUA ili kupunguza changamoto za udahili kwa vijana wanaohitaji kuijunga katika vyuo vikuu pamoja na kutoa elimu bora kwa watanzania.
“Nawapongeza sana SUA na MJNUAT kwa kufikia makubaliano haya ambayo kimsingi yatasaidia kuhakikisha kwamba MJNUAT inaenda kuanza mafunzo mwaka huu wa masomo” alisema Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini Mhe. Jumanne Sagini( Mb) amewataka wakazi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa zitokanazo na kufunguliwa kwa Chuo hicho Butiama kwa kuanzisha miradi mbalimbali.
“Siamini kama serikali itaweza kujenga majengo ya kuweza kuwachua watumishi wote watakaokwenda kule pamoja na wanafunzi kupata hosteli za kupanga kwa muda mfupi, hii iwe fursa kwa wananchi pamoja na mimi Mbunge wao nikiwemo, tuweze kujenga mambweni na nyumba za kuishi watu wote hao.” Alisema Mhe. Sagini
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia Prof. Lesakit Mellau amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira na miundombinu ya kujifunzia na tayari bilioni moja zimeshatolea.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema SUA imepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu hasa kuwanoa vijana katika nyanja mbaalimbali zikiwemo za sayansi ya kilimo hivyo makubaliano haya yatachagiza maendeleo katika sekta ya kilimo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here