Home BUSINESS NIC YAIBUKA KINARA TUZO YA SUPERBRANDS AFRIKA MASHARIKI KATIKA HUDUMA BORA ZA...

NIC YAIBUKA KINARA TUZO YA SUPERBRANDS AFRIKA MASHARIKI KATIKA HUDUMA BORA ZA BIMA

Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Karimu Meshack akionesha nembo ya tuzo ya Superbrands baada ya kuibuka kinara katika Mashirika yanayotoa Huduma bora za Bima katika ukanda wa afrika Mashariki.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.

Shirika la Bima la Taifa (NIC) limeibuka na ushindi wa Tuzo ya Superbrands Afrika Mashariki baada ya kuthibitika kuwa ndio Shirika linalotoa Huduma bora za Bima katika ukanda wa afrika Mashariki.

Aidha NIC imeendelea kung’ara Kimataifa kwa kupata cheti cha Ithibati katika utoaji wa Huduma  bora za Bima.

Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Karimu Meshack alipozungumza katika mahojiano maalum na waandishi wa habari katika Maonesho ya Biashara ya 47 ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema kwa mwaka huu Shirika hilo limechaguliwa kuwa Superbrands Afrika Mashariki, na kwamba Tuzo hiyo ni maalum kwa ajili ya Kampuni, Taasisi au Bidhaa inayotoa Huduma bora na ambapo wateja wenyewe ndio wanaotoa uthibitisho wa Bidhaa na Huduma bora wanayopata kutoka kwenye Taasisi husika.

“Sababu hizo zimepelekea sisi NIC kuibuka kinara wa huduma Bora, na kuwa kimbilio la watumiaji wa Huduma za Bima. Sasa ukishafikia hatua hiyo maana yake ndio unafikia vigezo vya kuchaguliwa kuwa ‘Superbrand’.

“Watanzania na wasio Watanzania ndio wametuchagua, hivyo basi NIC kwa kipindi hiki cha miaka minne imefanya mapinduzi makubwa kwa uendeshaji wa Kampuni hii ya Bima, katika utoaji wa huduma bora za Bima, kwani  tumewekeza kwenye wataalam wenye weledi na wanaokidhi vigezo vya utoaji wa huduma. amesema Meshack.

Ameongeza kuwa NIC imewekeza kwenye kutoa huduma kwa njia ya kisasa ya kidigitali na hivyo kuondokana na utaratibu wa zamani wa makablasha na badala yake kila kitu kinafanyika kwa njia ya mtandao kupitia mifumo ya Tahama.

“Hivyo basi uwekezaji huu umetufanya tulipe ndani ya siku 7 tofauti na zamani ambapo kwa mujibu wa mwongozo ilitakiwa tulipe ndani ya siku 45.

“Haya yote yamefanya kupata faida ya asilimia 100 kwa miaka minne mfululizo, wateja wameongezeka na mapato yameongezeka, hii imefanya sisi kuwa Kampuni Bora kabisa kuliko Kampuni yoyote ya Bima. Kwa mwaka jana tumepata faida ya shilingi bilioni 63.2 na tumeweza kupimwa kwa ukuzaji kwa asilimia 108, hakuna Shilika lolote la Bima ambalo limekuwa kwa kiwango hicho,”amesema Meshack.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here