Home BUSINESS MGODI WA BUCKREEF WAWAJENGEA UWEZO WAJASIRIAMALI WANAWAKE WILAYA YA GEITA

MGODI WA BUCKREEF WAWAJENGEA UWEZO WAJASIRIAMALI WANAWAKE WILAYA YA GEITA

Afisa Rasirimali watu Kutoka Mgodi wa Buckreef Domitilla Damas Akizungumza na wandishi wa habari katika mafunzo ya wajasiriamali wanawake wilaya ya Geita. Picha na Costantine James.

Meneja wa SIDO Mkoa wa Geita Nina Nchimbi akitoa mafunzo kwa wajasiriamali wanawake wilaya ya Geita. Picha na Costantine James

Baadhi ya wajasiriamali wanawake wakisikiliza mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na Mgodi wa Buckreef kwa kushirikiana na SIDO Mkoa wa Geita. Picha na Costantine James.

Na: Costantine James, Geita.

Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Buckreef kwa kushirikiana na SIDO Mkoa wa Geita imetoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake zaidi ya 250 ili kuwajengea uwezo wa kibiashara pamoja na mbinu za uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa zao ili kuweza kuzalisha bidhaa zenye tija kwa lengo la kuwainua kiuchumi.

Mafunzo hayo yamefanyika katika mji mdogo wa katoro wilaya ya Geita Mkoani Geita ambapo yamewakutanisha wajasiriamali wadogo wanawake kutoka kijiji cha Mnekezi kata ya Kaseme ambao wanapakana na Mgodi huo ili kuwapa elimu na ujuzi wa kuzalisha bidhaa zenye ubora zaidi.

Akizungumza katika Mafunzo hayo Afisa Rasirimali watu kutoka Mgodi wa Buckreef Domitilla Damas amesema mgodi huo umeamua kuwakutanisha wanawake hao ili kuwapa mafunzo na uelewa wa kufanya biashara na uzalishaji wa bidhaa ambazo wanaweza kupata fursa ya kuuza katika mgodi wa Buckreef ili kujiinua kiuchumi.

Amesema mafunzo hayo yanahusu uzalishaji na ufugaji wa kuku, mbuzi, ng’ombe, kilimo wa nafaka, mbogamboga na matunda ili kuwawezesha kupata fursa zinazopatikana katika mgodi huo kwa kuwapa mafunzo ya namna gani wanaweza kufanya kazi na mgodi na bidhaa zinazohitajika zaidi katika mgodi huo ili waweze kunufaika na uwepo wa mgodi katika maeneo yao.

Meneja wa SIDO Mkoa wa Geita Nina Nchimbi amesema wamewakutanisha wakina mama hao ili kuwajengea uwezo pamoja na kuwahamasisha kuunda vikundi mbalimbali na kuwapa elimu ya uongezaji thamani bidhaa zao ili kukidhi vigezo na waweze kuuza katika mgodi wa Buckreef na nje ya mkoa kwa lengo la kujipatia kipato.

Nina amesema pamoja na hayo wanawajuza fursa mbalimbali zinazo patikana katika mgodi huo ili waweze kuzichangamkia na kufaidika na uwepo wa mgodi huo katika maeneo yao huku akisema changamoto inayowakumba wajasiriamali wengi ni kukosa elimu juu ya uongezaji thamani wa bidhaa zao hali inayowakosesha masoko ya uhakika ya bidhaa zao.

Nao baadhi ya wakina mama walionufaika na mafunzo hayo wameupongeza mgodi wa Buckreef kwa kuwapa mafunzo hayo kwani awali walikua wanafanya biashara zao kimazoea na sasa wamejengewa uwezo ambao utawasaidia kukuza biashara zao pamoja na kuongeza wigo wa uzalishaji wa bidhaa zao.

Wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kuimalika zaidi katika biashara zao pamoja na uzalishaji wanaofanya huku wakiuomba mgodi huo kuendelea kuviwezesha vikundi hivyo kwa kuwapa mitaji pamoja na vitendea kazi ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora zaidi na zinazouzika kwenye masoko shindani ndani na nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here