Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeshauri vyama vya wafanyakazi ambavyo bado havijajiunga na Shirikisho la vyama hivyo (TUCTA), kujiunga ili kuleta ufanisi kwenye masuala ya wafanyakazi.
Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, Pendo Berege ambaye yupo chini ya Ofisi hiyo, amebainisha hayo Mei 16, 2023 kwenye mafunzo ya watendaji wa vyama hivyo, waajiri na shirikisho hilo yaliyofanyika Mjini Morogoro, yakilenga kukumbushana wajibu na majukumu katika utekelezaji wa katiba na kanuni za vyama.
Amesema katika vyama 33 vilivyosajiliwa, 13 vimejiunga na vyama 5 vimeingia katika mchakato wa kujiunga na TUCTA.
“Vyama vyote vikijiunga na TUCTA tutakuwa na uwezo wa kukaa kwa pamoja na kwa umoja wao kama watendaji wa vyama kujadiliana kuhusu haki za wafanyakazi kwenye maeneo ya kazi,’’ amesema.
Naye, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya amewataka viongozi wa vyama hivyo kuwafikia wanachama wao kwa wakati ili kuepusha migogoro isiyokuwa na lazima.
Amesema ili vyama vifanikiwe vinapaswa kuwa na nguvu ya kiuchumi ili wanachama wafikiwe kwa wakati wanapohitaji msaada.
Mwakilishi kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Leonard Selestine amesema suala la afya mahala pa kazi ni muhimu kuzingatiwa kwa wafanyakazi kwa kuwa linaongeza tija na uzalishaji kazini.
Aidha, amewataka wafanyakazi kuepuka vitendo na vishawishi vinavyosababisha rushwa mahali pa kazi, kujali muda na kutekeleza majukumu ya kazi inavyotakiwa.