Home LOCAL RAIS SAMIA AWAPA NENO MAKATIBU MAHUSUSI, AKIHITIMISHA MKUTANO WAO WA KITAALUMA ZANZIBAR

RAIS SAMIA AWAPA NENO MAKATIBU MAHUSUSI, AKIHITIMISHA MKUTANO WAO WA KITAALUMA ZANZIBAR

Zanzibar. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ameungana na viongozi wengine nchini kushuhudia kiapo kwa Makatibu Mahsusi na watunza kumbukumbu zaidi ya 8000 Tanzania kwa lengo la kulinda na kufanya kazi kwa weledi mahala pa kazi.

Historia imeandikwa Mei 27, 2023 katika viwanja vya Fumba mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar katika hitimisho la Mkutano wa Kumi wa Kitaaluma wa Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka uliofanyika kuanzia Mei 23 na kufikia kilele Mei 27, 2023.

Mhe.Dkt. Samia amesema kuwa sababu ya kuibua kundi hilo la Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbumbuku na Nyaraka ni kutokana na historia yake kipindi alipoanza kazi kama Mtunza Kumbukumbu hivyo anafahamu changamoto zipatikanazo katika sekta hiyo.

Aidha amesema kuwa, nidhamu, uadilifu na utunzaji siri mahala pa kazi ni eneo muhimu kwa mtumishi kwani inaleta ufanisi katika kazi na kuwa chachu ya kuleta maendeleo kitaaluma na nchi kwa ujumla.

Ameongeza kuwa malalamiko mengi yaliyoletwa na makundi hayo mawili Mawazili wenye dhamana wameyafanyia kazi na kuahidi kuwa suala la Mitaala litafanyiwa kazi kikamilifu ili nao waweze kupata nafasi mbalimbali za uteuzi mara baada ya kuongeza elimu.

Katika mkutano huo Makatibu Muhtasi na Watunza Kumbukumbu wote nchini wamekula kiapo cha utunzaji siri za ofisi, uadilifu , nidhamu warudipo makazini na kuwa wameandika historia nchini kwa kufanya hivyo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pia amewataka waajiri kuendelea kutoa ruhusa kwa Makatibu Mahsusi na watunza kumbukumbu kwa kufanya hivyo kunawaongezea weledi, kuwakumbusha majukumu yao katika kazi pamoja na kuwapa nafasi ya kutoka nje ya eneo la ofisi kupumzisha akili.

Vilevile kutokana na ushirikiano alioutoa Said Salim Bakresa kuandaa eneo kwa ajili ya kufanyika sherehe hizo amemuomba tena kujenga ukumbi wa mikutano katika viwanja vya Fumba utakaoweza kutoa huduma kwa mashirika mbalimbali kwa kutumia ukumbi huo.

Adha Rais Samia amewataka wageni wote waliofika Zanzibar katika Mkutano huo kutembelea maeneo ya Zanzibar akiamini wengi wao hawajawahi kufika Kisiwa hicho ili kuondoa dhana ya kuwa Zanzibar ni mji mdogo hivyo wafurahie na watembee waone ukubwa wa mji huo.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here