Home LOCAL JAMII INAHITAJI ELIMU ZAIDI MAKOSA YA KIMTANDAO – SSP MWANGASA

JAMII INAHITAJI ELIMU ZAIDI MAKOSA YA KIMTANDAO – SSP MWANGASA

Na: Mwandishi Wetu

MKUU wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Kimtandao Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, SSP Joshua Mwangasa amesema bado jamii inahitaji elimu ya kutosha kuhusu masuala ya kimtandao.

Mwangasa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa majadiliano ya utafiti kuhusu ‘Nafasi ya Haki za Kidijitali nchini Tanzania’ iliyoangazia uhuru wa kujieleza, faragha za wateja na utawala bora, uliowasilishwa na Taasisi ya Digital Agenda for Tanzania Intiative (DA4TI) kwa kushirikiana na Internews, USAID pamoja na Greater Internet Freedom.

“Kutokana na teknolojia inavyokuwa kila siku jamii inahitaji elimu kubwa ya masuala ya matumizi ya kimtandao na usalama wake kwa ujumla.Kwa hiyo sisi tunapongeza utafiti huu kwani ni jambo jema ambalo wamelifanya na tutaendelea kushirikiana nao.

“Kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala haya, kwani tunaamini wananchi wakipata elimu ya kutosha tutatatua changamoto hii kwa asilimia kubwa,” amesema SSP Mwangasa.

Awali akiwasilisha utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa DA4TI, Peter Mmbando amefafanua utafiti huo wameufanya katika nchi nne ambazo ni Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe huku kwa Tanzania wakiangalia kampuni ya Vodacom na Airtel.

Amesema lengo la kufanya utafiti huo ni kutafuta utatuzi wa changamoto ambazo zipo katika upande wa haki za kimtandao kwa kampuni za simu.”Tumefanya hivi ili kuongeza uanda mkubwa wa kufanya huduma ziwe bora zaidi zikilinda haki za binadamu.

“Na uhuru wa kujieleza na jinsi ambavyo mitandao ya simu wanavyochakata zile data kwaajili ya kulinda huduma za wateja…na hii itasaidia zaidi ili kufungua milango kwamba wanaweza wakaboresha huduma zao.

“Kwahiyo kikubwa zaidi ilikuwa ni watakavyolinda data na haki za kidijitali. Kwasababu tulichokibaini ni kwamba kwenye data katika upande wa privacy (faragha) kuna vitu havijawekwa na hakuna sehemu ya wateja kuripoti haki zao za kidijitali,” amesema Mmbando.

Aidha ametoa mwito kwa kampuni za simu kufanya marekebisho kwa ambapo waweke kipengele cha haki za kimtandao, wachapishe au kuziandika taarifa zao za miongozo kwa kiswahili.

“Kuwe na dawati maalum litakaloshughulikia masuala ya kimtandao, ambapo watu wataweza kuripoti kwani hii itasaidia sana sio taarifa zote ziende Customer Care (huduma kwa wateja) zingine ziwe katika kulinda haki madhubuti za watumiaji.”

Wakati huo huo mtaalamu wa masuala ya Privacy, Mrisho Swetu amepongeza utafiti huo ambapo ukifanyiwa kazi utakwenda kuondoa changamoto zilizopo katika masuala kimtandao.

“Sheria ya data ni pana sana tutakapoanza kuitumia itamgusa mmoja baada ya mwingine kwani changamoto zilizopo katika eneo hili ni nyingi sana,” amesema Swetu.

Mwisho

Previous articleRAIS SAMIA AWAPA NENO MAKATIBU MAHUSUSI, AKIHITIMISHA MKUTANO WAO WA KITAALUMA ZANZIBAR
Next articleTEMBO NICKEL KUANZA UZALISHAJI MWAKA 2026
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here