Home BUSINESS TEMBO NICKEL KUANZA UZALISHAJI MWAKA 2026

TEMBO NICKEL KUANZA UZALISHAJI MWAKA 2026

 Yathibitisha kutoa Fursa kwa Watanzania, hadi sasa imeajiri Watanzania 96

Kufikia Aprili 2023, Wakandarasi wametoa Ajira za muda mrefu kwa wafanyakazi 163

Manunuzi ya thamani ya Shilingi zaidi ya Bilioni 15 yamefanyika kwa watoa huduma wa kitanzania hadi kufikia Aprili, 2023

Asteria Muhozya na Steven Nyamiti – Dodoma

Imeelezwa kuwa, Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Ltd, inatarajia kuanza uzalishaji wa Madini ya Nikeli ifikapo mwaka 2026.

Hayo yamebainishwa na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nickel Benedict Busunzu katika Semina kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyoandaliwa na Wizara ya Madini kupitia kampuni ya Tembo Nickel kwa lengo la kuifahamisha kamati hiyo kuhusu shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo ikiwemo hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Busunzu amesema kutokana na umuhimu wa madini hayo katika matumizi mbalimbali ikiwemo matengenezo ya betri za magari, inatarajiwa ifikapo mwaka 2050, mahitaji ya madini hayo duniani yatakua ni zaidi ya mara nne ya mahitaji ya sasa.

Katika hatua nyingine Busunzu amesema, Kampuni ya Tembo Nickel inajivunia kuivutia kampuni kubwa duniani ya BHP ambayo baada ya kipindi cha miaka10 kutokufanya kazi Afrika, imerudi tena kupitia Tanzania ambapo hadi sasa imewekeza kiasi cha Dola za Marekani Milioni 100 katika mradi huo wa kuzalisha madini ya nikeli nchini.

Madini ya Nikeli hapa nchini yanatarajiwa kuchimbwa katika eneo la Kabanga, Wilayani Ngara Mkoa wa Kagera ambapo zaidi ya hekta 4,000 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa na wa aina yake nchini, barani Afrika na duniani.

Amesema pamoja na kuwepo kwa mgodi wa kuzalisha madini ya nikeli, pia, kutakuwa na kiwanda cha kusafisha madini hayo katika Wilaya ya Kahama na kueleza kuwa, eneo hilo lilipendekezwa kutokana na kuwa ni eneo la kimkakati na kutokana na uwepo wa miundombinu mbalimbali itakayosaidia mradi huo kutekelezwa kikamilifu na kama ulivyopangwa.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo kwa Tanzania tangu kuanza kutekelezwa amesema, tangu mwaka 2022 kampuni hiyo imekwishatoa kwa Serikali kiasi cha shilingi bilioni 12 kupitia kodi na malipo ya leseni na kuongeza kwamba, kwa kipindi cha mwaka 2023 pekee, manunuzi yaliyofanywa na kampuni hiyo kwa eneo la Ngara pekee yamefikia shilingi milioni 767 huku kiasi cha shilingi bilioni 15 kikiwa kimetumika kwa ajili ya watoa huduma mbalimbali wa ndani.

‘’Mhe. Mwenyekiti kipaumbele cha kampuni yetu ni kuona namna gani wananchi wa Ngara wananufaika zaidi na uwepo wa mradi huu. Hadi sasa tumetumia shilingi milioni 207 kwa huduma za kijamii na kiasi cha shilingi milioni 256 zimetumika katika maeneo ya miradi ya Afya, maji na elimu na maji ambayo kwetu yanaonekana ni muhimu,’’ amesema Busunzu.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu Rasilimali Watu Simon Sanga amesema hadi kufikia mwezi Aprili 2023, kampuni hiyo imeajiri wafanyakazi 103 watanzania wakiwa 96 huku kati yao wanawake ni 32 , wanaume 67 na wageni 4 na kuongeza kuwa, katika ajira za muda mfupi za kuanzia mwezi mmoja hadi mitatu, kampuni iliajiri wafanyakazi 667 kutoka maeneo yanayozunguka mradi.

‘’Wanufaika 10 wa programu ya vijana na kati yao asilimia 50 wametoka Kagera,’’ amesema Sanga.

Pia, amesema kwamba, wakandarasi wametoa Ajira za muda mrefu 163 na katika hizo watanzania ni 159 na wageni ni 4.

Naye Msimamizi wa Uhamishaji wa Watu na Makazi kutoka kampuni Kandarasi ya RSK Basil Shio Akizungumzia mpango wa kuhamisha watu na makazi amesema tayari kampuni hiyo imeanza kuandaa michoro ya nyumba za watu ambao nyumba zao zitaguswa na mradi na kwa upande wa waliopisha mradi, taratibu za fidia zinafanyika ikiwemo kuwaelimisha wananchi kutumia fedha za fidia kwa tija.

Januari 19 mwaka 2021 Serikali na kampuni ya LIfezone Metals Nickel Limited zilisaini Mikataba ambayo iliwezesha kuanzishwa kwa Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited ambayo ni ya ubia kati yake na Serikali. Aidha, mnamo mwaka huo huo tarehe 29 Oktoba, 2021 Serikali ilitoa Leseni kubwa ya uchimbaji wa madini ya Nikeli kwa kampuni hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here