Na: Irene Thompson
Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala ameitisha kikao kazi na wadau wa Usafi wa Mazingira wa Mkoa wa Dar es salaam kwa lengo la kupokea tathimini ya Kampeni ya *Safisha, Pendezesha Dar es salaam* iliyodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu na kupokea mikakati mipya ya Mkoa kwa ajili ya awamu ya pili itakayoanza…
Mhe. Makala ameelekeza watendaji kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Mitaa kuhakikisha zinadhibiti biashara holela, usafisha maeneo mbalimbali kwa kufanya usafi kila mwisho wa mwezi, kupanda miti na upendezeshaji wa barabara na kuweka sehemu stahiki za kuhifadhi takataka (dampo) kwenye kila wilaya ili kuondoa msongamano sehemu moja.
Pia, Mhe. Makala ametoa agizo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kushirikiana na Halmashauri za Mkoa wa Dar es salaam kuweka miundombinu ya maji kwenye bustani za barabarani ili kuondoka tatizo la miti kukauka msimu wa kiangazi.
“Usafi wa Mazingira unaendana sambamba na upatikanaji wa maji, DAWASA mtoe ushirikiano kwa Halmashauri wanapohitaji huduma za maji kwenye bustani zilizopo kwenye hifadhi za barabara ziwekewe mfumo wa umwagiliaji kuepuka kukauka kwa bustani hizo kipindi cha kiangazi.” amesema Mhe. Makala.
Mkuu wa Mkoa ameendelea kusisitiza wananchi kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa Mwezi ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.