Home BUSINESS TAASISI ZA SERIKALI ZIANDAE MIKAKATI YA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOIBULIWA KWENYE MIJADALA –...

TAASISI ZA SERIKALI ZIANDAE MIKAKATI YA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOIBULIWA KWENYE MIJADALA – DKT. ASHIL

Taasisi za Serikali zilizoshiriki Maadhimisho ya Siku ya Miliki Ubunifu zimetakiwa kuhakikisha kuwa mijadala iliyofanyika inawekewa mikakati bora ya kutatua changamoto zinazoibuliwa na wabunifu na wajasariamali ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa mujibu wa Sheria na kwa kujiamini zaidi hasa katika zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa kutambua kwamba Serikali inawathamini na kuhakikisha wanaongeza kasi ya Ubunifu katika kuendeleza bunifu na kukuza biashara zao.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, wakati wa ufunguzi wa maadhimisho yaliyoratibiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), katika Kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Dkt. Abdallah ameongeza kwa kusema kuwa katika maadhimisho hayo kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu, jambo zuri zaidi ni kwamba mijadala hiyo imehusisha wataalam na wadau mbalimbali katika sekta za umma na binafsi.

“Kunapokuwa na ushirikishwaji wa sekta binafsi ambao ni waendesha uchumi wa nchi katika shughuli za kiserikali na kuwa na mijadala mbalimbali, mara nyingi kunakuwa na uhalisia wa mijadala husika ambapo pande zote mbili yaani Sekta ya Umma na Binafsi zinakuwa na uelewa wa pamoja katika kutambua mafanikio na kubaini changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara hasa wajasiriamali”, ameongeza Dkt. Abdallah.

Amesisitiza kuwa kupitia jukwaa hilo ni vema kukawa na uelewa wa pamoja kuwa dunia ya sasa inalenga zaidi katika ukuaji na matumizi ya Ubunifu, Sayansi na Teknolojia, hivyo unapozungumzia Miliki Ubunifu unazungumzia Ubunifu, Sayansi na Teknolojia kama nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi.

Amesema pasipo kutumia Miliki Ubunifu, ukuaji wa uchumi wa Taifa lolote utayumba sana. Kuna mifano mingi hai ya nchi nyingi zilizoendelea na zimepata mafanikio makubwa ya kiuchumi kupitia Miliki Ubunifu kama vile nchi za Magharibi na Asia.

Awali Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Saudin Mwakaje ndiye aliyefungua mjadala ambao ulijadili mfumo wa usajili na ulinzi wa Miliki Ubunifu Tanzania, ambapo kupitia mada hiyo washiriki waliweza kujua Mifumo ya sajili mbalimbali zinazofanywa na BRELA, Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) na Chama cha Hakimiliki Zanzibar (COSOZA).

Kwa upande wa Ukiukaji na Utekelezaji wa Hakimiliki washiriki waliweza kufahamu namna haki za wabunifu zinavyowezwa kukiukwa. Mjadala huo uliongozwa na Bi. Neema Magimba Wakili kutoka Extent Corporate Advisory na kuchagizwa na wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Sheria kama vile Mahakama Kuu ya Tanzania, Kampuni ya Uwakili ya ABC na Tume ya Ushindani wa Haki (FCC).

Pia katika maadhimisho hayo wabunifu wa Alama za Biashara na Huduma pamoja na Hataza walitoa shuhuda za mafanikio katika matumizi ya Miliki Ubunifu pamoja na kuibua changamoto wanazokutana nazo. Shuhuda hizo ziliongozwa na Bi. Jeniffer Bash ambaye ni mmiliki wa Alama ya Alaska.

Baadhi ya Taasisi za Serikali zilizoshiriki katika maadhimisho hayo ni Mahakama Kuu ya Tanzania, Tume ya Ushindani wa Haki (FCC), Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), Chama cha Hakimiliki Zanzibar (COSOZA), Tume ya Sayansi na Teknonojia (COSTECH), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na BRELA ambao wameratibu maadhimisho hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here