Home LOCAL MRADI WA MAJI BILIONI 119 KUIFAIDISHA RUANGWA – MAJALIWA

MRADI WA MAJI BILIONI 119 KUIFAIDISHA RUANGWA – MAJALIWA

*Ashiriki kikao cha kutambulisha miaka miwili ya Rais Samia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inakuja na mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh. bilioni 119 ambao utahudumia vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na 21 vya wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

“Mradi huu ambao utaanzia Nyangao, kuja Nanganga hadi Ruangwa kisha utaenda Chiola hadi Nachingwea. Mkandarasi ameshapatikana na mkataba umeshasaIniwa. Kwa hiyo mradi utaanza wakati wowote,” amesema. 

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Machi 31, 2023) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Ruangwa waliohudhuria hafla ya kutambulisha mafanikio ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita iliyofanyika kwenye ghala la Lipande, wilayani humo.

“Dhamira ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuongeza uwezo wa upatikanaji wa maji kwenye miji yetu na vijiji vinavyozunguka miji hiyo.”

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, ametumia fursa hiyo kuelezea mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta za elimu, afya, maji, barabara, madini na michezo.

Kuhusu mafanikio ya elimu kwenye wilaya hiyo, Waziri Mkuu amesema miundombinu imeboreshwa kwa kujenga shule mpya za sekondari na za msingi, ufundishaji umeimarika na ufaulu kuongezeka na kufikia asilimia 98. 

Alisema wilayani humo kuna baadhi ya kata ambazo zina shule za sekondari mbili ambapo kata ya Likunja ina sekondari za Likunja na Kitandi. “Kata nyingine ni Narungombe kuna ambako kuna sekondari za Liugulu na Narungombe ambapo Liugulu tumeamua iwe ni maalumu kwa wasichana na Narungombe iwe maalumu kwa wavulana. “

Waziri Mkuu aliwapongeza walimu na wazazi kwa kuweza kudhibiti utoro wa wanafunzi na aliwapongeza wazazi kwa kusimamia nidhamu ya watoto wao na kufuatilia masomo yao. “Tukifanya haya, tutaongeza nguvu ya walimu na azma yetu ya kutoka asilimia 98 kwenda 100 itafikiwa,” amesema.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Bw. Abuu Jumaa ambaye alikuwepo kwenye hafla hiyo aliwataka wazazi wachukue tahadhari kwa watoto wao katika kipindi hiki ambacho kinakabiliwa na mmomonyoko wa maadili.

“Dunia imeharibika, sasa hivi kuna jambo la ushoga linaendelea. Nawaomba wazazi na wananchi wa Ruangwa tukae na watoto wetu na tulisemee jambo hili. Pia UKIMWI bado upo, tatizo la dawa za kulevya lipo, yote haya lazima tuyasemee kwa vijana wetu.

Naye, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel alikabidhi nyaraka za ununuzi wa dawa za mkoa mzima zenye thamani ya sh. bilioni 2 kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bibi Zainab Tellack ili aweze kuzifuatilia kwa makini kwa kila wilaya. Alisema mgao wa mkoa mzima ulikuwa sh. bilioni 6 lakini hadi sasa mkoa umeshatumia sh. bilioni 4.

Naye, Naibu Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange alisema Serikali inatambua kuwa Halmashauri hiyo ina upungufu wa magari ya wagonjwa na imeshalifanyia kazi suala hilo.

“Serikali imenunua magari matatu kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ambapo mawili kati ya hayo ni magari ya kubeba wagonjwa na gari moja ni la kusafirisha chanjo. Pia watumishi wa afya tumewaleta, wako 67 na walimu walioletwa hapa wako 91,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here