Home LOCAL MATOKEO YA SENSA YAMEONESHA TANZANIA IMEPIGA HATUA KIMAENDELEO-MAJALIWA

MATOKEO YA SENSA YAMEONESHA TANZANIA IMEPIGA HATUA KIMAENDELEO-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imeonesha Tanzania imepiga hatua katika kuwaletea maendeleo wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Maji, Elimu, Afya, na Mawasiliano.

Amesema hayo leo Jumamosi (Aprili 15, 2023) wakati alipozindua Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)-Tunguu. Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Seleman Abdulah.

Amesema kuwa katika Sekta ya Elimu, takwimu za Sensa zinaonesha kuwa kiwango cha jumla cha uandikishaji kwa wanafunzi ngazi ya shule za msingi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimefikia asilimia 95.9 Mwaka 2022 kutoka asilimia 94.6 ilivyokuwa Mwaka 2012.

“Kiwango cha kujua kusoma na kuandika kwa watu wenye umri wa miaka 5 na kuendelea kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimeongezeka hadi asilimia 79.1 mwaka 2022 kutoka asilimia 72.0 ilivyokuwa mwaka 2012”.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa sekta ya maji matokeo ya Sensa yanaonesha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufanya vizuri kwa kuwa asilimia 99.5 ya kaya zote zina vyanzo vya maji ambapo kati ya vyanzo hivyo asilimia 67.8 ni vyanzo vilivyoboreshwa na asilimia 32.2 ni vyanzo ambavyo havijaboreshwa.

Kwa upande wa mawasiliano, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 97.5 ya Vitongoji/Mitaa/Shehia vimefikiwa na mitandao ya simu. “Kiwango hiki kinafanana na hali ilivyo kwa Tanzania Bara. Wakati huohuo Tanzania Zanzibar imefanya vizuri zaidi kwa kufikia asilimia 99.0 ya shehia ambazo zimefikiwa na mitandao ya simu”.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote wapo kwenye umri wa miaka 15 hadi 64.

“Hii ni ishara nzuri katika maendeleo ya nchi, kidemographia umri huu unajulikana kama umri wa kufanya kazi Kwa maneno mengine, nchi yetu ina hazina kubwa ya nguvu kazi ambayo ni moja ya kichocheo katika kujenga uchumi imara”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa rai kwa wananchi kufuatilia kwa karibu taarifa za usambazaji wa matokeo haya na kuyatumia katika kufanya maamuzi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kubaini maeneo ya uwekezaji, upatikanaji wa huduma za kijamii na maeneo ya masoko kulingana na mtawanyiko wa idadi ya watu nchini.

Naye, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makazi Hemed Seleman Abdulah amesema kuwa Sensa ya mwaka 2022 ilikuwa tofauti na Sensa zote zilizopita kwani Serikali imelenga kutumia matokeo haya kuleta mafanikio na maendeleo makubwa ndani ya nchi yetu.

“Ili matokeo haya yaweze kufikiwa ni lazima takwimu hizi zitumike katika upangaji wa mipango ya maendeleo, ni imani yetu mipango yote ya maendeleo ya nchi yetu itahusisha takwimu za sensa hii ambayo imepita kila eneo la nchi yetu”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama amesema kuwa waitaitumia ripoti hiyo kama nyenzo muhimu ya kujenga ustawi wa watu na uendelevu wa Maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Naye, Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar Salum Kassim Ali amesema kuwa matumizi ya teknolojia yamesaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha ukusanyaji na uchakati wa taarifa zilizotokana na sensa ya watu na makazi hivyo kuwezesha kuongeza kasi ya utoaji wa matokeo ya Sensa kwa wakati.

Previous articleBODI YA UTALII YATOA MSAADA KWA JAMII
Next articleTMDA YAMNASA MTUHUMIWA WA MTANDAO WA UTENGENEZAJI DAWA BANDIA ZA BINADAMU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here