Home LOCAL WANANCHI KATIKA VIJIJI 12 BABATI WAMLILIA CHONGOLO MIGOGORO YA MIPAKA

WANANCHI KATIKA VIJIJI 12 BABATI WAMLILIA CHONGOLO MIGOGORO YA MIPAKA

Na: John Walter-Manyara.
Wananchi wa Vijiji 12 vya Halmashauri ya Babati vijijini vilivyo jirani na Hifadhi za Taifa ya Manyara na Tarangire wamemuomba Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo kuwapazia sauti kwa serikali ichukue hatua kutafuta suluhu ya mpaka kati yao na hifadhi hizo pamoja na kero ya wanyamapori kuingia kwenye makazi ya wananchi na kuleta uharibifu wa mali na maisha ya wananchi .
Diwani wa Kata ya Magara,wilayani Babati Jacob Fundi na Mbunge wa Babati Vijijini Daniel Sillo (CCM),wametoa ombi hilo kwa Chongolo aliyesimama kuzungumza na wananchi wa Magara akianza ziara yake wilayani Babati leo.
Akizungumzia mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi hizo na vijiji hivyo, Sillo amesema wananchi wana mgogoro wa mpaka baina yao na hifadhi hizo na haijawahi kupatiwa ufumbuzi.
Aidha amemuomba Chongolo kuwasaidia kufikisha kilio chao kwa serikali, ili wanyamapori wanaoingia vijijini humo kutoka kwenye hifadhi  hizo na kuharibu mazao yao walipwe fidia stahiki inayolingana na uharibifu uliofanywa.
Akijibu maombi hayo Chongolo amesema atazungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii,  ili aje kukaa na wananchi hao kuwasikiliza na wabainishe alama za mipaka ili kumaliza ugomvi.
“Ninakwenda kuzungumza na waziri husika aje hapa azungumze nanyi awaoneshe alama za mipaka halisi, lakini hili la wanyamapori wanapokuja kwa wananchi na kuleta uharibifu lazima mamlaka husika iwalipe fidia kulingana na uharibifu uliofanywa,” amesema Chongolo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here