WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona mabadiliko kwenye sekta ya mifugo si tu kwa kijiji cha Msomera bali kwa nchi nzima.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 7, 2023) wakati akizungumza na viongozi na wananchi waliohudhuria kikao cha siku moja alichokiitisha wilayani Handeni, mkoani Tanga ili kukabidhi rasmi mradi wa makazi maalum katika kijiji cha Msomera kwa Wilaya za Handeni na Kilindi.
“Serikali hii imesema eneo la Msomera litakuwa eneo la mfano kwa ufugaji wa kisasa na wa kibiashara. Kwa hiyo ni lazima tuweke utaratibu wa kufanya lionekane ni eneo la ufugaji wa kisasa,” amesema.
Kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni kwa sasa ni makazi ya wananchi ambao kuanzia Juni, 2022 walihama kwa hiyari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro ili kulinda ikolojia na uoto wa asili katika eneo hilo. Mara baada ya kuwasili, walipewa nyumba za kuishi za ukubwa wa vyumba vitatu kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 2.5 na jingine la malisho la ekari tano.
Ameziagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Wizara ya Mifugo ziweke utaratibu utakaowafanya wafugaji wafuge kitaalamu badala ya utaratibu wa mtu kuwa na mifugo mingi halafu anashindwa kuihudumia kwani utaratibu huo hauna tija.
“Wizara ya Mifugo pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI tengenezeni taratibu za kuonesha mfugaji wa Msomera mwenye ng’ombe 70 anafuga kwa tija zaidi kuliko mwenye ng’ombe 300. Hii inaweza kutumika hata kwenye mikoa mingine ambako kuna wafugaji,” amesisitiza.
Amezitaka Halmashauri za Mji Handeni na Wilaya za Handeni na Kilindi zinapoandaa bajeti zao kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha, zihakikishe zinaingiza mahitaji ya uendelezaji huduma kwenye kijiji cha Msomera ili kuimarisha ustawi wa wananchi wa kijiji hicho.
Pia amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wanapoenda kufanya ziara kwenye kijiji hicho wahakikishe wanaanzia kwanza kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kujitambulisha rasmi ndipo wapatiwe maafisa wa kuongozana nao.
Baada ya kupokea maswali na maoni kutoka kwa baadhi ya madiwani na malaigwanak, Waziri Mkuu aliwapa fursa Mawaziri na Naibu Mawaziri waliohudhuria kikao hicho watoe ufafanuzi wa masuala yaliyojitokeza yakiwemo ya maji, malisho na mawasiliano ya simu.
Mawaziri waliotoa ufafanuzi ni wa Maji, Maendeleo ya Jamii, Maliasili na Utalii na wa Mifugo na Uvuvi. Naibu Mawaziri ni wa Mambo ya Ndani, Habari, Mawasiliano na TEHAMA, Nishati, Ardhi na Maendeleo ya Makazi na wa TAMISEMI.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mkuu wa Majeshi, Makatibu Wakuu watano, Wakuu wa Mikoa ya Tanga na Arusha, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, wakuu wa taasisi, Madiwani, Malaigwanak, wawakilishi wa wananchi wa Msomera na watumishi wa Wilaya ya Handeni.