Home LOCAL TANZANIA NA AFRIKA KUSINI KUONGEZA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

TANZANIA NA AFRIKA KUSINI KUONGEZA MAENEO MAPYA YA USHIRIKIANO

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (BNC) kati ya Tanzania na Namibia, ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Fatma Rajab akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 13 hadi 16 Machi 2023.  

Katibu Mkuu Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini na Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (BNC) kati ya Tanzania na Afrika Kusini, Bw. Zane Dangor akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 13 hadi 16 Machi 2023.  

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na Katibu Mkuu Idara ya Uhusiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini, Bw. Zane Dangor wakifafanua juu ya utaratibu wa mkutano huo ambapo walieleza kuwa majadiliano ya mkutano yanafanyika katika makundi manne ambayo ni; Siasa na Diplomasia; Ulinzi na Usalama; Fedha na Uchumi, na Huduma za kijamii.

Pretoria, Afrika Kusini -13 Machi 2023

Tanzania na Afrika Kusini zimekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za fedha na uchumi, kilimo, madini, maji, utalii, siasa na diplomasia, mawasiliano na uchukuzi, teknolojia ya habari, uchumi, nishati, elimu, wiwanda, biashara na uwekezaji, ujenzi, utalii, kilimo, uvuvi, afya, elimu na utamaduni.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Bi-National Cooperation) kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaofanyika tarehe 13 – 16 Machi 2023 jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Mkutano huu uliofunguliwa katika ngazi ya Maafisa Waandamizi unafanyika tarehe 13 na  14 Machi 2023 pia ni mkutano wa awali kwa ajili ya kuandaa taarifa zitakazopitiwa na kujadiliwa na mkutano ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 15 Machi 2023. 

Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini unalenga kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa kwanza wa BNC uliofanyika mwezi Mei 2017 jijini Dar es salaam.

Akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini, ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Fatma Rajab ameeleza kuwa mkutano huu unatoa nafasi ya kupitia hali halisi ya utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa katika kikao cha kwanza na kuweka mikakati imara ya kusonga mbele kimaendeleo.

“Kikao hiki kitahusisha majadiliano yatakayowezesha kufikiwa kwa makubaliano katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano ya kisekta yatakayo rasimishwa kwa ajili ya utekelezaji na kuruhusu maeneo mapya ya ushirikiano” alisema Balozi Fatma.

Vilevile, akaeleza kuwa mkutano huu ni muhimu kwakuwa ushirikiano wa nchi zetu umejengwa katika misingi imara iliyopiganiwa kwa jasho na damu tangu enzi za ubaguzi wa rangi na hivyo BNC hiyo ni chachu ya kuimarisha na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika maeneo yatakayokubaliwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini na Mwenyekiti mwenza za kikao hicho Bw. Zane Dangor, alieleza kuwa BNC inatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji.

“Jukumu letu ni kuimarisha ushirikiano katika masuala yenye maslahi makubwa kwa mataifa yetu na kufungua fursa ya maeneo mapya ya ushirikiano” alisema Bw. Dangor.

Matarajio ya Wenyeviti wa Mkutano huu ngazi ya Maafisa Waandamizi ni kuhakikisha wajumbe wanawasilisha michango yenye tija ya kisekta katika majadiliano ili kuifikia hatua ya juu ya kimaendeleo kupitia ushirikiano uliopo.

Pia viongozi hao wamesisitiza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zinauchukulia kwa upekee ushirikiano huo kwakuwa nchi hizo zina masuala mengi ya kushirikishana kupita uanachama wake katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika – SADC na kwa lengo la kujenga uchumi wa kanda hiyo na Afrika kwa ujumla.

Tanzania na Afrika Kusini zilikubaliana kuanzisha Tume ya Marais ya Uchumi (Presidential Economic Commission-PEC) mwaka 2005 na mwaka 2011 nchi hizo zilisaini Tume ya Ushirikiano wa Pamoja (Bi-National Commission) ambayo ilichukuwa nafasi ya PEC.

 Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.

Previous articleSPIKA DKT. TULIA AKIHUTUBIA MKUTANO MKUU WA IPU BAHRAIN
Next articleHOTUBA – MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MAFUNZO KWA WAKUU WA WILAYA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here