Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, leo tarehe 29 Machi, 2023 akielezea kuhusu mchango unaotolewa na vyombo vya habari kufikisha taarifa za BRELA kwa jamii, katika Mkutano wa mwaka wa Kitaaluma wa Wahariri wa Vyombo vya Habari (TEF), unaofanyika mjini Morogoro.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa akisisitiza jambo alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya Whariri katika mkutano huo.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Mnauye (Mb), akimkabidhi cheti cha shukrani Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, leo tarehe 29 Machi, 2023 katika Mkutano wa mwaka wa Kitaaluma wa Wahariri wa Vyombo vya Habari (TEF), unaofanyika mjini Morogoro. BRELA ni miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizotoa mchango kufanikisha mkutano huo.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imewapongeza Wahariri wa Vyombo vya habari kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwa BRELA katika kuwafikia wadau popote walipo kupitia vyombo vya habari.
Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw.Godfrey Nyaisa, ametoa pongezi hizo katika mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioanza leo tarehe 29, Machi,2023 Mjini Morogoro na kueleza kuwa jitihada hizo zimesaidia kuongeza uelewa wa wadau kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA.
“Nikiri kwamba, Vyombo vya Habari hasa ninyi Wahariri mmekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya BRELA, ambapo mmewezesha wafanyabiashara kutumia huduma zinatolewa na Wakala za kurasimisha biashara na kupata ulinzi wa Miliki Ubunifu pamoja na Leseni, hii imetokana na jitihada zenu za kutoa habari mbalimbali zinazohusu BRELA bila vikwazo vyovyote”, amesema Bw. Nyaisa.
Aidha Bw. Nyaisa ameongeza kuwa kupitia vyombo vya habari, wananchi wameelewa mifumo inayotumika kufanya sajili mbalimbali ikizingatiwa kwamba sajili zote zinafanyika kwa njia ya mtandao na kuchangia ongezeko la sajili na utoaji wa Leseni za Biashara kundi “A”.Mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS) na mfumo wa Tanzania National Business Portal (TNBP).
Kutokana na mafanikio hayo Bw. Nyaisa ameeleza kuwa kwa mwaka 2023 BRELA imepanga kukutana na Wahariri ili kujadili na kukubaliana namna bora ambayo itawezesha kushirikiana katika eneo la uwezeshaji wa biashara nchini na kudumisha zaidi uhusiano uliopo.
Vilevile, ameongeza kuwa BRELA itatoa mafunzo kwa waandishi wenye weledi wa kuandika habari za biashara, kuhusu huduma inazozitoa na kwa kuanzia, mafunzo hayo yatatolewa kwa waandishi wa mkoa wa Dar es Salaam.
Akifafanua zaidi Bw. Nyaisa amesema kutokana na uelewa wa wananchi kuongezeka kumekuwa na ongezeko la Sajili kwani katika kipindi cha miaka miwili yaani mwaka 2021 mpaka 2023, BRELA imeshuhudia ongezeko la idadi ya sajili za kibiashara na utoaji wa Leseni ambapo Kampuni za Kitanzania 13,663 zimesajiliwa sawa na ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na Kampuni 10,790 zilizosajiliwa mwaka 2021.
Ameeleza pia kuwa Kampuni za Kigeni 93 zimesajiliwa sawa na ongezeko la asilimia 29 ikilinganishwa na Kampuni za kigeni 72 zilizosajiliwa mwaka 2021.
Kwa upande wa Majina ya Biashara 25,507 yamesajiliwa ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na Majina ya Biashara 21,836 yaliyosajiliwa mwaka 2021.
Vilevile amesema Alama za Biashara na Huduma 3,607 zimesajiliwa ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na Alama za Biashara na Huduma 3,137 zilizosajiliwa mwaka 2021. Pia kwa upande wa Leseni za Biashara kundi “A” 13,663 zimetolewa ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 13 ikilinganishwa na Leseni 10,790 zilizotolewa mwaka 2021.
Mkutano wa 12 wa Mwaka wa Kitaaluma wa Wahariri unaofanyika kwa siku nne nne, umefunguliwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe.Nape Nnauye (Mb), kaulimbiu ya mkutano huo ni “Sheria za Habari na Maendeleo ya Vyombo vya Habari “.
Mwisho