Home BUSINESS BoT YATOA TAMKO LA KAMATI YA SERA YA FEDHA

BoT YATOA TAMKO LA KAMATI YA SERA YA FEDHA

Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ilikutana tarehe 14 Machi 2023, kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha katika miezi Januari na Februari 2023,   Fax No. 2234217 

mwenendo wa uchumi, na kufanya maamuzi ya mwelekeo wa utekelezaji wa sera ya  fedha kwa miezi miwili ijayo. Kamati iliridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha  iliyolenga kupunguza ongezeko la ukwasi kwenye uchumi ili kukabiliana na kasi ya  mfumuko wa bei nchini. Kufuatia utekelezaji thabiti wa sera ya fedha, mfumuko wa bei  umeendelea kubakia ndani ya malengo, na kiwango cha ukwasi kikiendana na  mahitaji halisi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi, hali iliyochochea ongezeko la  ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, na kuweka mazingira ya kuendelea kuimarika  kwa shughuli za kiuchumi nchini. Vilevile, utekelezaji huu wa sera ya fedha umesaidia kufikiwa kwa vigezo vilivyowekwa katika makubaliano ya programu na Shirika la  Fedha la Kimataifa (IMF) chini ya Mpango wa Extended Credit Facility (ECF) kwa  mwezi Desemba 2022, na kuendelea kupunguza athari za kiuchumi zitokanazo na  mitikisiko ya kiuchumi duniani, hususan athari za ongezeko la bei za bidhaa katika  soko la dunia. 

Kuhusu mwenendo wa uchumi, Kamati ilibaini kuwa mwaka 2022 uchumi wa dunia uliathiriwa na mitikisiko ya kiuchumi na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.  Kutokana na haya, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia inatarajiwa kupungua mwaka  2023, kabla ya kuongezeka tena mwaka 2024. Bei za bidhaa katika soko la dunia  ziliendelea kuwa juu katika mwaka 2022, japo zilianza kupungua katika kipindi cha  nusu ya pili ya mwaka. Kutokana na hali hiyo, mfumuko wa bei umeendelea kupungua  tangu robo ya mwisho ya mwaka 2022, japo umebaki juu ya malengo ya benki kuu za  nchi nyingi, hususan mataifa yaliyoendelea. Aidha, Kamati ilibaini kuwa: 

  1. Mwenendo wa uchumi nchini umeendelea kuwa wa kuridhisha, huku viashiria  mbalimbali vya shughuli za kiuchumi vikionesha matarajio chanya kwa kipindi  kijacho. Kwa kuzingatia kasi ya wastani wa ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.2  katika robo tatu za kwanza za mwaka 2022 kwa Tanzania bara, kuna  

uwezekano mkubwa ukuaji wa uchumi ukafikia asilimia 5 kwa mwaka 2022,  kiwango ambacho ni juu ya makadirio ya awali ya ukuaji wa asilimia 4.7. Kwa  upande wa Zanzibar, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.4 mwaka 2022,  kutokana na jitihada zinazoendelea katika kuimarisha uchumi wa buluu,  kuimarika kwa shughuli za utalii, pamoja na sera madhubuti za fedha na  kibajeti. Kamati inatarajia ukuaji wa uchumi kuendelea kuimarika zaidi ndani ya  mwaka 2023 kutokana na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, jitihada  mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira  ya biashara na uwekezaji nchini, kuimarika kwa shughuli za utalii, na utekelezaji  wa sera madhubuti za fedha na kibajeti. Hali hiyo itachagizwa pia na matarajio  ya kupungua kwa shinikizo la mfumuko wa bei na kuimarika kwa mnyororo ya  ugavi duniani; 

  1. Mfumuko wa bei umeendelea kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni,  kutokana na athari ya vita inayoendelea nchini Ukraine, ambayo imesababisha ongezeko la bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi. Mfumuko wa bei  kwa Tanzania bara uliongezeka na kufikia asilimia 4.9 mwezi Januari 2023,  kutoka asilimia 4.8 mwezi uliotangulia, kiwango ambacho kimeendelea kubakia ndani ya lengo la nchi la asilimia 5.4 kwa mwaka 2022/23, na vigezo vya  mtangamano vya nchi wanachama wa EAC na SADC vya asilimia 8 na asilimia  3 hadi 7, mtawalia. Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei uliongezeka na  kufikia asilimia 8.4, kutokana na ongezeko la bei za chakula na bidhaa zisizo  za chakula. Aidha, Kamati inatarajia mfumuko wa bei nchini kubaki ndani ya  lengo katika nusu ya pili ya mwaka 2022/23 kutokana na matarajio ya  kuendelea kupungua kwa bei za bidhaa na mfumuko wa bei katika nchi  washirika wa biashara, pamoja na matarajio ya kuongezeka kwa uzalishaji wa  mazao ya chakula nchini. Kupungua huku kutachagizwa pia na utekelezaji  thabiti wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kiwango cha ongezeko la  ukwasi kwenye uchumi unaofanywa na Benki Kuu; 

iii. Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 12.8 katika  mwaka ulioshia Januari 2023, sanjari na lengo la asilimia 10.3 kwa mwaka  2022/23. Hali hii ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ukuaji mzuri wa mikopo kwa  sekta binafsi uliofikia takriban asilimia 23; 

  1. Katika miezi saba ya kwanza ya mwaka 2022/23, utekelezaji wa bajeti za  Serikali umeendelea kufanyika kuendana na malengo. Mapato ya ndani 

yalifikia asilimia 97.1 na asilimia 96.1 ya malengo kwa Tanzania Bara na Zanzibar, mtawalia. Mwenendo huu umechangiwa na kuimarika kwa mifumo  ya usimamizi wa ukusanyaji mapato na utayari wa walipa kodi. Aidha, matumizi  ya Serikali yalifanyika kulingana na rasilimali zilizopo, sanjari na uhitaji wa kuimarisha miundombinu nchini na jitihada za Serikali za kuunusuru uchumi  kutoka katika athari za misukosuko ya kiuchumi duniani kwa lengo la  kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi na endelevu; 

  1. Sekta ya nje imeendelea kuathiriwa na misukosuko inayotokana na vita inayoendelea nchini Ukraine na athari za janga la UVIKO-19. Changamoto hizi zilipelekea kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na  uhamisho mali nchi za nje, kufikia dola za Marekani bilioni 5.2 mwaka ulioishia  mwezi Januari 2023, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 2.6  mwezi Januari 2022, kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa katika soko  la dunia. Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 4.8 mwishoni  mwa mwezi Januari 2023, kiwango kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na  huduma kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.3, ikilinganishwa na lengo la nchi la  miezi isiyopungua minne. Katika vipindi vijavyo, urari wa biashara ya bidhaa,  huduma na uhamishaji mali nchi za nje, pamoja na idadi ya miezi ya uagizaji  wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, vinatarajiwa kuimarika kutokana na  kuendelea kuimarika kwa mnyororo wa ugavi na matarajio ya kupungua kwa  bei za bidhaa katika soko la dunia; 
  2. Sekta ya benki imeendelea kuwa thabiti, yenye kiwango cha kutosha cha mitaji,  ukwasi, na yenye kutengeneza faida. Rasilimali za sekta ya benki na amana  ziliendelea kuongezeka kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi,  pamoja na ongezeko la matumizi ya huduma za uwakala wa mabenki na  huduma za fedha kidijitali. Aidha, rasilimali za sekta ya benki zimeendelea  kuboreshwa, zikiakisiwa na kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu hadi  kufikia asilimia 5.85 mwezi Januari 2023, kutoka asilimia 8.42 mwezi Januari  2022; 

Kwa kuzingatia mwenendo na matarajio ya uchumi wa ndani na nje ya nchi, Kamati  ya Sera ya Fedha imeridhia Benki Kuu ya Tanzania kuendelea na utekelezaji wa sera  ya fedha inayolenga kupunguza kiwango cha ukwasi katika uchumi kwa mwezi Machi  na April 2023. Msimamo huu wa sera ya fedha unalenga kuhakiksha kuwa mfumuko 

wa bei unabakia ndani ya lengo la asilimia 5.4, na kuendelea kuchochea kuimarika  kwa shughuli za uchumi nchini. Vilevile, sera hii ya fedha itasaidia kufikiwa kwa  malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF chini ya mpango wa ECF kwa  mwezi Machi na Juni 2023. Aidha, Benki Kuu itaendelea kuweka mazingira ya kisera  yatakayowezesha kufikiwa kwa malengo mapana ya kiuchumi ya Serikali, na kufuatilia 

kwa karibu mwenendo mzima wa vihatarishi mbalimbali vinavyotokana na misukosuko  ya kiuchumi duniani, na kuchukua hatua stahiki pale itakapohitajika. 

GAVANA 

BENKI KUU YA TANZANIA

Previous articlePAP YAENDESHA WARSHA YA MAFUNZO KWA WABUNGE JUU YA USIMAMIZI WA UHAMIAJI BARANI AFRIKA
Next articleKAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA UTEKELEZAJI MIRADI YA AFYA RRH-IRINGA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here