Na: Elimu ya Afya Kwa Umma, Dodoma
Naibu Waziri Wizara ya Afya Dkt.Godwin Mollel Dkt .Godwin Mollel amesema Bima ya Afya kwa Wote itakuwa suluhisho ya kuondoa changamoto zilizopo kwa CHF hivyo ni muhimu kila mwananchi kujiandaa kunufaika vifurushi vitakavyopatikana kupitia bima hiyo pindi itakapoanza.
Dkt.Mollel amebainisha hayo leo Februari 20, 2023 jijini Dodoma katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri pamoja na taasisi za sekta ya Afya unaoratibiwa na Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo unaokwenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Uboreshaji wa Huduma za Afya ni Nguzo ya Kufikia Afya kwa Wote ”
“Tulichowaambia Waganga wakuu kuwa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote utakuwa mwarobaini wa kuondoa matatizo ya ubovu uliopo ndani ya CHF “amesema.
Kuhusu ubora wa Huduma Dkt.Mollel amesema umeimarika kutoka asilimia 72% hadi asilimia 81% kupitia vituo mbalimbali vya kutolea huduma za Afya.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof.Abel Makubi amekumbusha uongozi wa kuleta matokeo chanya katika utendaji huku akizungumzia umuhimu wa kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi katika sekta ya Afya.
“Katika Uongozi wa Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika utendaji lazima tuwe na viongozi wanaojitambua ,kuratibu mambo na kusimamia vyema katika Sekta hii ya Afya kuanzia Zahanati na hili suala la changamoto ya watumishi ni lazima tutatue matatizo ya ajira katika sekta ya Afya naambiwa kuna zaidi ya madaktari 3000 wapo mitaani,zaidi ya wauguzi 20,000 wapo mitaani,ni lazima tuyatatue haya matatizo” amesisitiza Prof.Makubi.
Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa Tanzania Dkt.Best Magoma amezungumzia mafanikio katika sekta ya afya kuwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ambapo serikali ilishatoa Tsh.Bilioni 123 .53 za ruzuku kuendeleza ujenzi wa hospitali 135 na kukarabati hospitali kongwe .
Naye Kaimu Mkurugenzi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma,Idara ya Kinga Wizara ya Afya Dkt.Tumaini Haonga amesema Elimu ya Afya kwa Umma itaendelea kuongeza nguvu kwa kutumia redio jamii katika kuelimisha Umma kuhusu masuala mbalimbali ya Afya ikiwemo elimu Jumuishi huku msisitizo zaidi juu ya uchunguzi wa Magonjwa ya awali .
Pia Dkt.Haonga amesema Elimu ya Afya kwa Umma imekuwa ikituma wataalam wenye Ubobezi kwa ajili ya Elimu ya Afya Shuleni.