Home LOCAL ATAKAYEMZUIA MWANAFUNZI KUPATA ELIMU KUCHUKULIWA HATUA-MAJALIWA

ATAKAYEMZUIA MWANAFUNZI KUPATA ELIMU KUCHUKULIWA HATUA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Mchinga, Mama Salma Kikwete, Bungeni jijini Dodoma.

Waziri Mkuu, Kassi Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Madiwani kutoka jiji la Tanga kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Februari 10, 2023.  Kushoto kwake ni Mbunge wa Tanga Mjini na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI  Mkuu  Kassim Majaliwa amesema Serikali haitosita kumchukulia hatua mzazi au mtu yeyote atakayemzuia mwanafunzi kupata haki yake ya elimu, hivyo amewataka wazazi wote wenye wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza kuhakikisha kuwa watoto hao wanaripoti kwenye shule walizopangiwa mara moja.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 10, 2023) wakati akiahirisha Mkutano wa 10 wa Bunge la 12, Bungeni Jijini Dodoma. Waziri Mkuu ametumia fursa hio kuziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo bado hazijakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kuhakikisha vyumba hivyo vinakamilika.

Mheshimiwa Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilitoa shilingi bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 8,000 vya madarasa katika shule za sekondari ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023.

Waziri Mkuu amesema hadi kufikia tarehe 03 Februari 2023 vyumba vya madarasa 7,874 sawa na asilimia 98.43 vimekamilika na vyumba vya madarasa 126 sawa na asilimia 1.57 vipo katika hatua mbalimbali za umaliziaji.

“Ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa ya sekondari umewezesha wanafunzi wote 1,076,037 waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2022 kupata fursa ya kupangiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwezi Januari 2023 kwenye shule za Serikali kwa awamu moja pekee.”

“Mafanikio haya ni kielelezo tosha cha umakini, uzalendo, maono na kazi iliyotukuka inayotekelezwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulinda maslahi na kujenga mustakabali mzuri wa Taifa letu.”

Akizungumzia kuhusu uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na awali,Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kufanya vizuri ambapo hadi kufikia tarehe 03 Februari, 2023 wanafunzi 1,363,320 wa darasa la awali wameandikishwa wakiwemo wenye mahitaji maalum 2,944 sawa na asilimia 100.18 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,360,737.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi hicho wanafunzi 1,657,533 wakiwemo wenye mahitaji maalum 3,825 waliandikishwa kwa ajili ya darasa la kwanza sawa na asilimia 101.29 ya wanafunzi 1,633,659 waliotarajiwa kuandikishwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kudhibiti matumizi ili kuendana na mpango na bajeti ya 2022/2023, ambapo ametumia fursa hiyo kuielekeza Wizara na taasisi zote za Serikali kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/2024 katika maandalizi ya bajeti za mafungu husika.

Waziri Mkuu amezielekeza Halmashauri zote nchini zenye mapato yasiyolindwa chini ya shilingi bilioni mbili (Kundi C), zihakikishe zinatenga kiasi kisichopungua asilimia 20 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikijumuisha asilimia 10 ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu;

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wote wa Mikoa wahakikishe wanasimamia kwa karibu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili miradi hiyo iweze kuakisi thamani ya matumizi ya fedha za umma.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaelekeza  Maafisa Masuuli wote wazingatie kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/2024 ikiwa ni pamoja na kuzingatia kikamilifu Sheria ya Bajeti (SURA 439) na Kanuni zake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here