Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeipongeza Wizara kwa jitihada mbalimbali ilizozifanya katika kutatua changamoto ya upungufu wa sukari nchini ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023 na kuitaka kuongeza nguvu kuondoa changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula na mchele.
Aidha, Kamati hiyo imeiagiza Wizara kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (MKUMBI) kwa wakati ili kurahisisha ufanyaji biashara na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza nchini ili kukuza biashara na uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. David Mwakiposya Kihenzile wakati Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara ikiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu yake pamoja na ya Taasisi zake 16 kwa Kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2022 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Nao Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni mbalimbali yaliyolenga kutatua changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula na mchele, kutafuta masoko ya nje ya bidhaa mbalimbali ikiwemo bidhaa za mwani, uendelezaji wa maeneo maalumu ya kiuchumi, mifuko ya uanzishaji wa biashara ndogo, fursa za soko la AfCFTA na uanzishaji wa mfuko wa ubunifu.
Naye Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara imepokea mapendekezo na maoni yote yaliyotolewa na itayafanyia kazi ili kuendelea kuweka mazingira bora na wezeshi ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kukuza uchumi wa Taifa.
Akiwawilisha taarifa hiyo mbele ya Kamati, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Ally Gugu amesema katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2022 Wizara imeendelea kutekeleza jitihada mbalimbali katika kuendeleza sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara
Amesema jitihada hizo ni pamoja uanzishaji wa mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma za pamoja, uendelezaji wananchi kiuchumi, utekelezaji wa miradi ya kimkakati, uratibu wa mahusiano ya kibiashara kikanda na kimataifa pamoja na upitiaji wa sera na sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Uwekezaji 2022,